RAIS John Magufuli amesisitiza azma yake ya kujenga Tanzania mpya, kwa kutangaza ajira 3,000 katika Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ujenzi wa reli ya kisasa ya umeme kipande cha Morogoro hadi Dodoma na yeye kuhamia Dodoma mwakani.
Alisema hayo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Jijini Arusha baada ya kutunuku Kamisheni kwa Maafisa Wanafunzi wapya 422 wa jeshi wa cheo cha Luteni Usu wa Kundi la 61/16, Miongoni mwa maafisa hao wapya, 32 ni wanawake na wanaume ni 390 ikiwa ni mara ya kwanza zoezi hilo kufanyika katika jiji la Arusha ambapo awali lilikuwa likifanyika katika chuo cha kijeshi cha Monduli ama Jijini Dar Es Salaam.
Wanafunzi waliotunukiwa vyeo hivyo, wanatoka Shule ya Anga, Shule ya Ubaharia na Chuo cha Kijeshi cha Monduli. Baada ya kutunukiwa vyeo vipya, maafisa hao wapya walikula kiapo cha utii mbele ya Rais Magufuli na baada ya hapo ofisa mpya, Sikujua Peter alivalishwa bawa kwa niaba ya marubani wenzake.
Awali, Rais Magufuli alitoa zawadi kwa mwanafunzi aliyefanya vizuri Shule ya Kijeshi ya Kibaharia, Jacob Soka, waliofanya vizuri darasani ni Ally Kitawala na Hamza Msuya, huku Benjamin Fanuel alipata zawadi kutokana na kufanya vyema katika masuala ya urukaji katika anga. Waliofanya vizuri zaidi katika Shule ya Kijeshi ya Monduli ni Hamis Mwantega, aliyefanya vizuri darasani ni Haji Kimaro.
Wanafunzi hao waliotunukiwa vyeo hivyo vipya, walipita mbele ya Rais kwa gwaride la mwendo wa pole na kasi, huku wakishangiliwa na watu mbalimbali waliofika uwanjani hapo kushuhudia kutunukiwa kwa kamisheni zao.
“Kwa kutambua hilo natangaza rasmi nafasi 3,000 za kuajiri wanajeshi wapya. Na hao watakaoajiriwa wawe wamemaliza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Lengo ni tuwe na maaskari wa kutosha na jeshi la kisasa zaidi,” alisema Rais Magufuli, ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu.
Alipongeza JWTZ, Polisi, Zimamoto, Uhamiaji, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCB) na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, kwa kazi nzuri ya kulinda amani ya nchi pia Alitaka wananchi kuendelea kuunga mkono vyombo hivyo.
Kuhusu suala la ajira, Rais alisema katika mwaka huu wa fedha, serikali inatarajia kuajiri jumla ya watumishi 50,000 wa sekta mbalimbali, ikiwemo wanajeshi, madaktari na walimu.
Kuhamia Dodoma, Rais alisema uamuzi wa kuhamia Dodoma kutoka Dar es Salaam, ulitolewa na Serikali ya Awamu ya Kwanza ya Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1973, lakini kwamba tangu wakati huo utekelezaji wake ulikuwa mgumu. Lakini, alisema serikali yake imedhamiria kuhamia Dodoma na kwamba hadi sasa watumishi 3,000 wamehamia Dodoma akiwemo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Aidha Rais alisema uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi na Tanzania ni moja ya nchi tatu barani Afrika, zinazoongoza kwa uchumi kukua, ya kwanza ikiwa ni Ethiopia ambapo uchumi wa Ethiopia unakua kwa asilimia 8, wakati wa Tanzania unakua kwa asilimia 7.1 na mwakani utakua kwa asilimia 7.2 sawa na wa India.
Viongozi walioshuhudia wanajeshi hao wapya wakitunukiwa vyeo ni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhani, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hussein Mwinyi, Mbunge wa Ngorongoro William ole Nasha, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, wakuu wa wilaya za Arusha na wakurugenzi wa wilaya.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa