Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Suleiman Jaffo (MB) amesema kuwa kituo cha Afya Murriet kilichopo katika kata ya Murriet Jijini Arusha ndio kituo pekee cha mfano kati ya vituo 350 vipya vya afya vinavyojengwa hapa nchini.
Waziri Jaffo ameyasema hayo wakati wa ziara yake Jijini Arusha leo Tarehe 09/11/2018 alipotembela kituo hicho cha afya kilichoanza kutoa huduma kwa wananchi mwanzoni mwa juma hili pamoja na kukagua mendeleo ya ukarabati na ujenzi wa baadhi ya majengo katika kituo cha afya Kaloleni ulioanza Tarehe 19/09/2018 kama alivyoelekeza wakati wa ziara yake aliyoifanya mwezi Septemba mwaka huu.
Pia ametoa rai kwa waganga wafawidhi wa vituo vipya nchini kuhakikisha wanaboresha mazingira kwa kutengeneza bustani zitakazowezesha vituo kuwa na mandhari ya kupendeza na kuwawezesha wananchi kuona kama hospitali ni sehemu ya utalii.
"Nawapongeza viongozi wa Mkoa wa Arusha akiwemo Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya , Mkurugenzi , Mganga Mkuu, mhandisi wa Jiji na wengine kwa kusimamia vyema kazi za ujenzi wa vituo vya afya na hiki Kituo cha Murriet ni mfano mzuri. Na kwa hapa nchini tayari vituo vya afya vipya 210 vimekamilika katika miezi 18 na vingine vinajengwa na kufikia idadi ya 350 hivyo nilishaomba Bohari ya Dawa (MSD) kuhakikisha wanapeleka dawa kwa wakati katika vituo vya afya " alisema Waziri Jaffo
Pia amemuagiza Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Murriet, Bw. Mustafa Miraji kuhakikisha upatikanaji wa dawa kwa wananchi usiwe kikwazo na kamwe kusitokee malalamiko kwa wananchi kuhusu utoaji wa huduma bora ya afya kwani serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais wake Dkt. John Pombe Magufuli imedhamiria kwa dhati kushughulika na matatizo ya wananchi ikiwemo changamoto ya huduma za afya
Aidha Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Mrisho Gambo amesema kuwa kituo hicho kina zaidi ya watumishi 27 wa afya ambao wametoka katikati hospitali mbalimbali na vituo vingine vya Afya vilivyopo Jijini hapa hivyo serikali ipo katika mchakato wa kuongeza watumishi wengine katika kituo hicho na vingine ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa watumishi wa afya utakaojitokeza kutokana na uhamisho huo.
Ujenzi wa kituo cha afya Murriet ulianza Mwaka 2017 na mpaka sasa umegharimu zaidi ya Shilingi Milioni 986, ujenzi umekamilika kwa jengo la wagonjwa wa nje na liko tayari kutumiwa na wananchi na huduma zimeanza kutolewa ikiwemo huduma ya mama na mtoto, huduma ya wagonjwa wa nje (opd), maabara, dawa na chanjo.
Utolewaji wa huduma za afya katika kituo cha Murriet kutasaidia kutatua changamoto za huduma za afya kwa wakazi wa kata ya Murriet na Jiji zima kwani utaimarisha hali ya utoaji wa huduma za afya na kupunguza msongamano katika hospitali na vituo vingine vya afya vilivyopo Jijini Arusha
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa