Siku ya UKIMWI duniani imeadhimishwa kiwilaya katika viwanja vya TBA Jijini Arusha Tarehe 2/12/ 2019 na mgeni wa heshima akiwa ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqarro. Kauli mbiu ya maadhimisho ikisema “JAMII NI CHACHU YA MABADILIKO TUUNGANE KUZUIA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU” .
Katika maadhimisho hayo watu wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI wamegawiwa Jumla ya kadi 95 za bima ya Afya na Mhe.Gabriel Daqarro pamoja na zawadi kwa washindi walioshiriki mashindano ya michezo iliyofanyika katika maadhimisho hayo.
Akisoma risala kwa mgeni rasmi katika sherehe hizo Ndg.Tumaini Abdala kwa niaba ya vijana wanaoishi na virusi vya UKIMWI alisema huduma kwa watu wanaoishi na VVU imeboreshwa kwa kiasi kikubwa kwani upatikanaji wa dawa kwa sasa ni wakuridhisha pia msongamano kwa baadhi ya vituo vya kutoa huduma umepungua kwa kiasi kikubwa hivyo kupunguza idadi ya vifo vitokanavyo na ukosefu wa huduma hizo muhimu.
Hata hivyo vijana hao wameainisha changamoto zinazo wakabili kuwa ni ukosefu wa dawa za kuzuia magonjwa nyemelezi, kipato duni, ukosefu wa lishe bora na kunyanyapaliwa .
Akizungumza katika maadhimisho hayo Mhe.Daqarro ametaja kwa asilimia kasi ya maambukizi ya virusi vya VVU nakusema kuwa kwa Tanzania bara maambukizi ni asilimia 4.7 ambapo katika Jiji la Arusha kwa mwaka 2015 maambukizi yalikua ni kwa asilimia 4.1, 2016 ni asilimia 3.6, 2017 ni asilima 2.8 na 2018-2019 ni asilimia 2.2 hivyo taarifa hizi zinaonyesha kwamba maambukizi yanapungua kwa kiasi kikubwa na amewashukuru wadau wote wanaoongoza mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU chini ya ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji.
Sambamba na hayo Mhe.Daqarro ameiasa jamii kwamba kushuka kwa kiwango cha VVU haimaanishi kuwa hakuna UKIMWI kwani katika Jiji la Arusha zaidi ya watu 35,000 wanamaambukizi na kati ya hao watu 8000 wameacha kutumia dawa na wapo miongoni mwa wana jamii hivyo jitihada ziendelee kufanywa za kuwakumbusha walioacha kutumia dawa watumie ikiwezekana watafutwe popote walipo.
Akihitimisha Mhe.Daqarro amesema takwimu zinaonyesha kuwa kati ya vijana wa umri kati ya miaka 15 hadi 24 ndio wenye maambukizi mapya hivyo waratibu wa Afya na wadau mbalimbali waendeshe semina katika shule na vyuo kwani katika kupambana na VVU ni muhimu kukemea vitendo viovu na hatarishi kwa yatima na watoto walioko katika mazingira magumu.
Mwisho.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa