Halmashauri ya Jiji la Arusha leo Tarehe 24/06/2019 imetia saini mkataba mpya na kampuni ya BQ CONTRACTORS LTD ya jijini Dar Es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa jengo jipya katika hospitali ya wilaya ya Arusha iliyopo kata ya Engutoto wenye gharama ya sh. Bilioni 1.3
Jengo hilo litajumuisha wodi ya wazazi, watoto na upasuaji na linatarajiwa kumalizika ifikapo Januari mwaka 2020.
Wakati wa hafla fupi ya utiaji saini wa mkataba huo Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni alimuagiza mkandarasi kutekeleza mradi huo kwa wakati ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika hospitali na vituo vya afya vilivyoko katikati ya mji.
Akishuhudia utiaji saini wa mkataba huo mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqarro amesema kuwa awali serikali ilitenga kiasi cha fedha sh. Milioni 535 kwa ajili wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na wananchi wanaendelea kupatiwa huduma.
“Tangu kuanzishwa kwa jiji la Arusha hakujawahi kuwa na hospitali ya wilaya hivyo nipongeze juhudi za Rais wa awamu ya tano Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuendelea kuipa kipaumbele sekta ya afya” alisema Mhe. Daqarro.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya BQ CONTRACTORS LTD Bw. Silas Bura ameahidi kukamilisha ujenzi huo kwa wakati na ameishukuru halmashauri ya jiji la Arusha kwa kutoa kipaumbele kwa wakandarasi wazawa ili kutekeleza mradi huo mkubwa na muhimu kwa wananchi.
Mwisho.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa