Na Mwandishi Wetu
Arusha
Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya OR-TAMISEMI imeandaa mpango Shirikishi wa Kuthibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ikiwemo kichocho na minyoo tumbo kwa shule za msingi ili kulinda usalama wa mtoto na makuzi yao.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Wilaya ya Mpango huo, Mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda amesema kuwa baadhi ya wanafunzi wanaathirika na minyoo hivyo Serikali imeleta dawa hizo kwa lengo la kuhakikisha usalama wao.
Aidha Mhe. Mtanda amesema kuwa magonjwa ya minyoo huwa hayapewi kipaumbele katika jamii hivyo wazazi wanatakiwa kuhakikisha watoto wao wanameza vidonge hivyo ambapo zoezi hilo linatarajiwa kuanza rasmi Novemba 18 hadi 19,2022.
"Wanaohusika ni wanafunzi wote wa shule za msingi wanatakiwa kumeza vidonge kwa ajili ya kukinga magonjwa yatokanayo na minyoo hivyo wito wangu kwa walimu wa shule za msingi,Maafisa elimu kata wanatakiwa kuhakikisha wanafunzi wote wenye umri wa miaka 5 hadi 14 wanapata dozi ya vidonge,"amesema Mtanda.
Kwa upande wake Mratibu wa Mpango Shirikishi wa Kuthibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele Jiji la Arusha Bi. Monica Ngonyani amesema mpango huo ni shirikishi wa kudhibiti magonjwa ambayo hayapewi kimpaumbele ikiwa magonjwa hayo ni mabusha,matende,trakoma,usubi ,kichocho na minyoo tumbo.
Aidha amesema kuwa Halmashauri ya Jiji hilo iliingia mkataba tangu Februari 22, 2022 yenye jumla ya bajeti ya Sh. milioni 58.5 ambazo ni ruzuku kutoka kwa wafadhili RTI kwa msaada wa watu wa marekani kwa lengo la kufanikisha zoezi hilo.
"Shughuli zinazofanywa katika zoezi hilo ni pamoja na mafunzo kwenye ngazi mbalimbali,shughuli za uhamasishaji kwa njia ya gari,redio,usimamizi shirikishi ma ufuatiliaji na ukusanyaji wa taarifa,"amesema.
Amesema kuwa wanatarajia mwaka huu kufikia asilimia 100 endapo wakipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa watu mbalimbali hadi kukamilika kwake Novemba 19,2022.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa