Na Mwandishi Wetu
Arusha.
Halmashauri ya Jiji la Arusha imetoa kiasi cha Shilingi Milioni 33 kwaajili ya kununua unga lishe maalum kwaajili ya watoto wenye mahitaji maalum waliopo mashuleni katika Halmashauri hiyo lengo likiwa ni kuwaongezea afya ya mwili na akili kwa watoto hao.
Akikabidhi unga huo pamoja na vifaa vingine kwenye shule za msingi 9 ambazo zina idadi ya watoto 519 wenye mahitaji maalum Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Bw. Hargeney Chitukuro amesema Serikali kupitia Halmashauri hiyo imefikia hatua hiyo ya kutoa vyakula vyenye lishe kwa watoto hao wenye mahitaji maalum ili wazidi kukua kiafya na waweze kukuza taaluma zao wawapo madarasani.
"Naishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaangalia watoto hawa wenye mahitaji maalumu ili kupata haki zao za msingi ikiwemo elimu. Hawa watoto wanahitaji kukua kiakili na kimwili, pia wanahitaji vifaa mbalimbali vya kuwasaidia watoto hawa". amesema Chitukuro.
"Sisi kama Jiji la Arusha tumesema tutaendelea kuwasaidia watoto hawa katika nyanja mablimbali ikiwemo ya miundombinu mashuleni ili iwe rafiki kwa watoto wetu hawa wenye mahitaji maalum". ameongeza Chitukuro.
Aidha Chitukuro ameeleza kuwa swala kuwanyanyapaa watoto wenye mahitaji maalum halitakuwa sawa maana nao pia wanavipawa kama watu wengine na wanaweza kuwa bora zaidi katika taifa hili na kulisogeza mbele katika hatua mbalimbali.
"Niwaombe wazazi kuendeleza upendo kwa watoto hawa wenye mahitaji maalum tusiwafiche tuwatoe waje wachanganyikane na wengine kwenye kupata elimu bora nao wanayo nafasi ya kuifanyia jambo nchi yao maana wanavipawa vyao". alisema Chitukuro.
Kwa upande wake Afisa Mwandamizi kutoka Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia Idara ya elimu maalumu Ndg. Seleman Chamshama amesema wao kama Wizara wanaendelea kuhakikisha watoto wote wenye mahitaji maalum hapa nchini wanajiunga na masomo na tayari Serikali inaendelea kuwaboreshea miundombinu ya elimu wawapo mashuleni.
"Yapo mahitaji mengi kwa watoto hawa ikiwamo sare za shule, viatu, madaftari n.k niwaombe watanzania wenzangu wenye kuguswa na hili waweze kuwasaidia watoto hawa ili waweze kupata mahitaji kama walivyo wengine kwasasa Serikali tunahakikisha wanapata elimu ambayo itawasaidia na kukuza vipawa vyao". amesema Chamshama.
"Niwaombe watanzania wengine wenye uwezo waweze kujitoa kuisaidia Serikali kuwasaidia watoto wenye mahitaji maalum maana changamoto ni nyingi Serikali peke yake haitaweza kumaliza ila kwa kushirikiana kwa pamoja tutaweza". aliongeza Chamshama.
Aidha Chamshana aliipongeza Ofisi ya Mkurugenzi Jiji la Arusha kwa kutoa fedha za kuwanunulia chakula chenye lishe watoto wenye mahitaji maalum kwa shule 9 ambazo zote zimepata unga huo pamoja na vifaa vingine ambazo zinajumla ya wafunzi 519 ambao niwanufaika wa msaada huo. Pia amewapongeza wazazi wote waliyo watoa watoto wao ndani na kuwapeleka shuleni kupata elinu.
Akishukuru kwa niaba ya walimu wakuu wa shule hizo 9 Mwalimu Mkuu wa Shule ya msingi Kaloleni Mwalimu Miminini Payema ameishukuru Serikali kupitia Mkurugenzi wa Jiji la Arusha kuguswa na kutoa chakula chenye virutubishi vyote vitakavyo saidia watoto kukua kiakili na kimwili.
"Sisi kaloleni mpaka sasa tunao wanafunzi 128 wenye mahitaji maalum tunao wahudumia kuwapatia elimu hii ya msingi niwaombe wazazi wawalete watoto wenye mahitaji maalum ili waje wachanganyikane na wenzao kupata elimu sisi walimu tupo tayari kuwapokea na kuwapatia elimu bora". Amesema Mwl. Payema.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa