Halmashauri ya Jiji la Arusha leo Tarehe 30 Octoba 2018 imeweka historia kwa kufanya mahafali ya pamoja kwa wanafunzi wa kidato cha nne wa shule zote za sekondari za serikali na binafsi zilizopo Jijini Arusha.
Mahafali hayo ya kihistoria yalioandaliwa na uongozi wa Jiji la Arusha kwa kushirikiana na wakuu wa shule zote za serikali na binafsi pamoja na wadau mbalimbali wa elimu, yamelenga zaidi kutoa fursa kwa wanafunzi ambao shule zao hazifanyi mahafali kutokana na uchumi duni ambao unawakwamisha kuchangia gharama kubwa za uendeshaji wa mahafali hayo pamoja na kutoa fursa kwa wanafaunzi wanaohitimu kuzijua fursa wanazoweza kuzitumia baada ya kumaliza masomo ya sekondari ikiwa ni kujiendeleza kiuchumi, kijamii na kiteknolojia hasa kwa wale watakaokosa nafasi za kuendelea na kidato cha tano.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo ambapo aliipongeza kamati ya maandalizi ya mahafali hayo kwani ni ya kipekee kuwahi kutokea katika halmashauri zote hapa nchini.
Mhe. Gambo alisema kuwa wazazi wengi wamepata muamko wa kuwapeleka watoto wao shule baada ya mpango wa serikali wa Elimu Bila Malipo kuwapunguzia wazazi na walezi gharama za kusomesha watoto wao hivyo katika kukabiliana na changamoto ya uchache wa madarasa katika baadhi ya shule serikali imetenga shilingi Bilioni 3 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ambapo Bilioni 1.5 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na Bilioni 1.5 nyingine ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za sekondari.
“Nichukue fursa hii pia kuwapongeza walimu, wanafunzi na wazazi au walezi kwa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ambapo Halmashauri ya Jiji la Arusha imeshika namba moja Kitaifa na Mkoa wa Arusha kushika namba tatu kimikoa” alisema Mhe. Gambo
(Pichani: Mmoja wa wahitimu wa elimu ya kidato cha nne (kushoto) akipokea cheti kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo katika mahafali ya pamoja kwa wanafunzi wa kidato cha nne wa shule zote za sekondari za serikali na binafsi zilizopo Jijini Arusha yaliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Jijini Arusha leo Tarehe 30 octoba, 2018)
‘’Niwatakie kila la kheri wanafunzi wote mnaotarajia kufanya mitihani ya kumaliza Elimu ya Sekondari Tarehe 05 Novemba 2018 na katika mkoa huu nitahakakikisha tunakwepa vitendo vya udanganyifu katika mitihani kwani vinaweza kutuletea fedheha ya kufutiwa mitihani na kuharibu sifa nzuri tuliyonayo katika Mkoa wetu” aliongeza mkuu wa mkoa huyo.
Naye Afisa Elimu Sekondari Bw. Valintine Makuka ameipongeza Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Magufuli kwa mpango kabambe wa Elimu Bila Malipo tangu aingie madarakani mwaka 2015. Kwa upande wa Jiji la Arusha hadi kufikia Juni 2018, Halmashauri ilikuwa imepokea jumla ya Shilingi 1,018,247,376.99 ikiwa ni fedha ya ada na ruzuku za uendeshaji.
Bw. Makuka ameongeza kwa kusema kuwa mahafali hayo yatasaidia kutoa mwamko wa hamasa kwa wazazi na wadau wa elimu katika kuchangia maendeleo ya elimu kwa kushirikiana na Jiji la Arusha kama waraka wa Serikali Na. 6 wa 2015 unavyoeleza majukumu ya jamii na wazazi. Moja Ya changamoto kuu ni chakula cha mchana.
(Pichani: Baadhi ya viongozi na wadau wa Elimu wa Jiji la Arusha waliohudhuria katika mahafali ya pamoja kwa wanafunzi wa kidato cha nne wa shule zote za sekondari za serikali na binafsi zilizopo Jijini Arusha yaliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Jijini Arusha leo Tarehe 30 octoba, 2018)
Mahafali hayo ya aina yake yaliyofanyika katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid uliopo Jijini Arusha ulijumuisha zoezi la ugawaji wa vyeti na zawadi kwa wahitimu pamoja na walimu waliofanya vizuri katika kufundisha masomo yao pia wamiliki wa vyuo na taasisi mbalimbali walipata nafasi ya kuwaonyesha wahitimu fursa zilizopo katika shughuli za kujiendeleza katika nyanja mbalimbali za kiuchumi .
Mahafali hayo yanatariwa kufanyika kila mwaka katika Halmashauri ya Jiji la Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa