Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo amempongeza Eng. Samuel Mshuza, Kaimu Mhandisi wa Jiji kwa hatua nzuri ya ujenzi wa kituo cha afya Murriet ulipofikia na pia amewaagiza kuwa ifikapo Tarehe 30 ya mwezi huu ujezi wa kituo hicho uwe umekamilika na huduma kwa wananchi zianze kutolewa mara moja.
Ameyasema hayo hapo jana alipokuwa katika ziara yake ya Afya Jijini hapa ambapo alipata fursa ya kutembelea vituo vya afya Murriet na Moshono pamoja na hospitali ya wilaya ya Arusha mjini iliyopo kata ya Engutoto.
Wakati wa ziara yake katika ujenzi wa hospitali ya wilaya iliyopo kata ya Engutoto Mkuu wa Mkoa alisema kuwa serikali kwa kutambua umuhimu wa afya kwa wananchi wake imetenga kiasi cha fedha sh. Milioni 535 kwa ajili wa ujenzi huo wa hospitali ya wilaya.
“Katika upande wa dawa serikali imefanikiwa kutenga kiasi cha fedha cha sh. Milioni 800 katika jiji la arusha ambapo hali ya upatikanaji wa dawa ni sawa na 98% ukilinganisha na hapo awali ambapo serikali ilikuwa ikitenga kiasi cha sh. Milioni 400 sawa na asilimia 49% ya upatikanaji wa dawa” alisema Mhe. Gambo.
Sambamba na ziara hiyo pia mkuu wa mkoa alipata fursa ya kusikiliza kero za wananchi waishio kata ya olasiti ambapo kilio chao kikubwa kwa serikali ni uhaba wa umeme, maji na barabara.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kwa Jiji kubwa kama la Arusha ni aibu kupatikana baadhi ya maeneo yenye uhaba wa upatikanaji wa huduma ya maji umeme na miundombinu mibovu ya barabara hivyo atashirikiana na wataalamu waliopo Jijini hapa na kutatua changamoto zinazowakabili kwa muda mrefu.
“Serikali ya awamu ya tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr. John Pombe Magufuli imeikabidi mamlaka ya maji safi na maji taka mkoani hapa (AUWSA) zaidi ya sh. Bilioni 476 kuhakikisha upatikanaji wa huduma hiyo unakuwa ni wa uhakika pia katika Jiji letu” alisema mhe. Gambo wakati wa mkutano huo
Pia alitoa nafasi kwa wataalamu wa kutoka taasisi mbalimbali ikiwemo Wakala wa Barabara za Mijini na vijijini (TARURA), Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Arusha (AUWSA) kwa ajili ya kutoa ufafanuzi juu ya changamoto zilizoanishwa na wananchi hao ambapo kwa upande wake Ndg. Fodia Mwankenja, Meneja wa TARURA alisema tayari wameshakubaliana na viongozi wa kata hiyo kutembelea mtaa wenye changamoto ya kivuko cha waenda kwa miguu na kuahidi uwa ujenzi utaanza mara moja endapo watajiridhisha kuwa hali ya barabara inapitika.
Wakati akifunga mkutano huo Mkuu wa Mkoa aliahidi kutoa mifuko ya simenti 100 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko hicho utakapoanza .
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa