MKUU wa Wilaya ya Arusha Gabriel Daqarro amewaomba wanawake kutowaamini watoto wa kiume wa ndugu zao na kuwaachia watoto wao kulea ili kupunguza idadi ya matukio ya vitendo vya ubakaji na ulawiti vinavyoshamiri wilayani humo.
Ombi hilo alilitoa leo jijini Arusha wakati akizungumza na akina mama wakati wa maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ambayo kitaifa yalifanyika Machi 8 na kwa upande wa Halmashauri ya Jiji la Arusha yameadhimishwa Machi 9 mwaka huu.
Alisema familia nyingi zinakumbwa na matukio hayo sababu ya kuwaamini kupita kiasi watoto wa mjomba,dada na ndugu wengine, jambo ambalo kwa sasa kila mmoja anapaswa kuacha na kuchukua tahadhari.
"Mimi nawaomba akina mama acheni kabisa kuamini watoto wa ndugu kwani matukio mengi ya ubakaji na ulawiti yanafanywa na watoto wa ndugu, tena ikiwezekana chukueni tahadhari hata kwa baba wa hao watoto wenu maana wengine baadhi wanabaka na kuwalawiti watoto wao wa kuwazaa
yaani msiamini mtu kupita kiasi,"alisema.
Aidha aliwasihi wanawake kusaidiana kurudisha jamii kwenye maadili kwani yameporomoka kuzidi kiasi.
"Mi hapa napo nawaomba tusaidiane kuwarudisha watoto wetu kwenye kuwajenga kiroho kwa kuwahimiza kwenda nyumba za ibada kanisani au msikitini kutegemea na imani ya kila familia kwa kufanya hivi itatusaidia sana kujenga taifa lenye hofu ya Mungu na kuwa na maadili mema katika jamii,"alisema.
Pia alikemea jamii za wafugaji pembezoni mwa Jiji kuacha kubagua watoto kwa kusomesha watoto wa kiume pekee na kudharau wakike.
Daqarro alisema ni vema kila mtu akafahamu mtoto wa kike akisoma jamii nzima imeelimika na asilimia kubwa ndio viongozi wazuri wa baadaye na waangalizi wa familia tofauti na watoto wa kiume.
Alisisitiza lazima kila familiya ikazingatia usawa wa kijinsia na kukemea mila na desturi zilizopitwa na wakati.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Chama cha Mapimduzi (UWT) Mkoa wa Arusha, Yasmin Bachu aliwaomba wanawake kupendana na kuacha chuki miongoni mwao ili wasaidiane kushika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi mkuu mwaka huu.
"Mwaka huu kuna uchaguzi mkuu jitokezeni kugombea nafasi mbalimbali na nawaomba tumpe heshima Rais John Magufuli katika uchaguzi wa mwaka huu, tusirudie makosa ya mwaka 2015 tuliyofanya,"alisema.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa