Maafisa Maendeleo Jiji la Arusha watakiwa kupinga Ukatili
Na Mwandishi wetu
Maafisa maendeleo wa Kata katika Halmashauri ya Jiji la Arusha wametakiwa kutumia nafasi zao vyema kwa kuhakikisha kuwa wanapinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika kata wanazofanya kazi lengo ikiwa ni kujenga jamii bora ambayo inatambua haki za binadamu na kuzilinda.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Dk.John Pima wakati akifungua mafunzo ya maafisa wa maendeleo kutoka kata 25 wa Halmashauri hiyo mafunzo yenye lengo la kuwajengea uwezo wa namna bora kusaidia jamii kupinga ukatili wa kijinsia na umuhimu wa Lishe bora kwa watoto.
Dk.Pima alisema kuwa maafisa maendeleo wanajukumu lakuhakikisha kuwa watoto hawatendewi ukatili wa kijinsia katika jamii wanazofanyia kazi kwa kuchukua hatua za kisheria kwa watu watakaobainika wanaonyanyasa watoto.
Pamoja na mambo mengine anawataka kuhakikisha wanaelimisha jamii kuhusu Lishe bora kwa watoto ikiwa ni kuwaepushia watoto magonjwa yanayoweza kutokea kutokana na kukosa lishe bora
Kwa upande wake Kaimu Afisa Maendeleo ya Jamii Halmashauri ya Jiji la Arusha Hanifa Ally alisema kuwa mafunzo hayo ya siku mbili kwa maafisa maendeleo kutoka kata 25 za Halmashauri ya Jiji la Arusha yana lengo la kuwakumbusha na kuwajengea uwezo maafisa hao juu ya Ukatili wa watoto na Lishe bora.
Bi Hanifa alisema kuwa maafisa hao wanajukumu la kuhakikisha kuwa ukatili katika kata zao unakomeshwa na kujenga jamii bora isiyokuwa na uonevu.
Anaongeza kuwa maafisa hao wanapaswa kuhimiza Lishe bora kwa watoto, kwa kuwa lishe bora ni matokeo ya ukuaji bora wa watoto na kwamba jamii inatakiwa kuelimishwa umuhimu wake na hatimaye kuweza kuwahudumia watoto kwa kuwapatia mlo kamili.
Hanifa alisema kuwa mafunzo hayo yanalengo la kuwajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za wananchi ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia kwa kuhakikisha kuwa wahanga wa ukatili wanapata msaada wa kisheria pindi inapobainika kuna ukatili.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha kupitia idara ya maendeleo ya Jamii ikiwa ni kuwajengea uwezo wa kusaidia jamii kupinga ukatili wa kijinsia na namna ya kuhimiza Lishe bora kwa watoto katika jamii.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa