Na Mwandishi Wetu
Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuachana na siasa zisizo na tija badala yake waungane kwa pamoja katika kuleta maendeleo ya wananchi wa Jiji hilo.
Mhe. Mtahengerwa ameyasema hayo katika Mkutano wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wa robo ya tatu ya mwaka 2022/2023 ambapo amewataka pia madiwani hao kutokuwa wapingaji wa mawazo ambayo yanatolewa kwa maslahi mapana ya Halmashauri hiyo.
Aidha, Mhe. Mtahengerwa amewataka madiwani hao kusimamia miradi inayotekelezwa na Halmashauri hiyo na kutatua changamoto zilizopo kwani Baraza hilo lina mamlaka ya kusimamia vizuri mambo yote ambapo pia ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kubakikisha wanasukuma ajenda ya maendeleo katika Jiji la Arusha.
Sambamba na hayo, Mhe. Mtahengerwa amewataka viongozi hao katika mikutano yao kwa kushirikiana na makanisa na misikiti kwa umoja wao kukemea vitendo vya ulawiti na ushoga ndani ya jamii na kuwaomba wazazi kukaa na watoto wao kujua mwenendo wa maisha yao na kuwafanya marafiki ili kukitokea tofauti waweze kuwaeleza mapema.
Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa Wilaya ya Arusha ipo katika mchakato wa kuzikagua taasisi binafsi na shule za kulelea watoto maarufu kama Day Care kama havikiuki maadili ya jamii na nchi na endapo vitabainika kuwa vinachochea ongezeko la vitendo vya ulawiti na ushoga vitafungwa na wahusika kuchukuliwa hatua kali za kisheria mara moja.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Hargeney Chitukuro akijibu swali la papo kwa papo katika Baraza hilo amesema kuwa suala la vitambulisho vya wazee viendelee kutambuliwa na kufanyiwa kazi kwenye maeneo ya upatikanaji wa huduma katika hospitali na vituo vya afya na kuongeza kwamba kupuuziwa kwa vitambulisho hivyo katika maeneo ya utoaji wa huduma ni ukiukwaji wa sheria na kwamba jambo hilo watalifanyia kazi.
Naye Diwani wa Kata ya Ngarenaro na Mwenyekiti wa Kamati ya huduma za Jamii katika Halmashauri ya Jiji la Arusha Mhe. Isaya Doita ameahidi kufanyia kazi maelekezo ya Mkuu wa Wilaya aliyoyatoa kwa maendeleo ya Jiji ili kabla ya kumalizika kwa mwaka mwaka huu wa fedha wawe wameweka mikakati itakayoleta tija kwa wananchi wa Arusha Jiji.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa