Na Mwandishi wetu
Baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa nchini kuwapanga vema machinga, Halmashauri ya Jiji la Arusha imeanza kutekeleza maelekezo hayo ambapo, Leo September 23,2021 Baraza la madiwani la Jiji hilo limefanya kikao cha dharura chenye lengo la kupitisha bajeti ya ujenzi wa maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya machinga.
Baraza hilo limepitisha bajeti ya Shilingi za Kitanzania Billioni 1 kwa kuanzia ambapo utekelezaji wa mradi huo utaanza na eneo moja baada jingine huku fedha hizo zikitolewa kwa awamu.
Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya machinga ni eneo la NMC Samunge, eneo lilopo jirani na stendi ya daladala Kilombero, eneo la Machame luxury, eneo la kiwanja namba 68 Kilombero, eneo la kwa Mrombo na eneo la uwanja wa Ulezi (Florida).
Akizungumza wakati wa Baraza hilo la Madiwani Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maxmillian Iranqhe amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa maelekezo kwa Wakuu wa Mikoa nchini kuwapanga vema machinga, nakueleza kuwa baada ya utekelezaji wa maelekezo hayo Jiji la Arusha litakua katika mpangilio mzuri na wenye kuvutia.
Mhe. Iranqhe amesema Arusha ni Jiji la kitalii na uchumi wake hutegemea sekta hiyo kwa kiwango kikubwa, hivyo amesisitiza kuwa utekelezaji wa maelekezo hayo ya Mheshimiwa Rais ni hatua kubwa ambayo itaimarisha uchumi wa Jiji hilo, kwani ni hatua itakayowakaribisha watalii wengi kwa kuvutiwa na mpangilio mzuri wa Jiji , huku hatua hiyo ikidhamiriwa kuwa miongoni mwa jitihada za wazi zitakazojenga hadhi ya Jiji la Arusha inayosifika kwa majina kama 'Geneva of Africa' na California ya Tanzania.
Aidha Mhe. Iranqhe amesema mradi huo utakapokamilika machinga wataondoka barabarani, wataondoka kwenye mitaro ya maji na kuacha ujenzi holela kwenye maeneo ya 'Central Business District' (CBD).
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. John Pima ametoa wito kwa machinga wa Jiji la Arusha kuwa watakaopangwa kwenye maeneo yaliyotengwa ni wale ambao wana vitambulisho vya machinga, huku akielekeza utaratibu wa kujipatia vitambulisho hivyo kuwa ni kuanzia kwenye ofisi za Kata ambapo watafanyiwa tathmini ya uhalali wa kukidhi vigezo vya kuwa machinga.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sekei Mhe. Gerald Sebastian amesema ujenzi wa maeneo hayo kwa ajili ya machinga utasaidia kurasimisha na kuwatambua machinga wa Jiji la Arusha, huku Diwani wa Kata ya Lemara Mhe. Naboth Selasie akieleza kuwa mradi huo utakapokamilika utaboresha maisha ya wananchi.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa