Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha Mhandisi Juma Hamsini amewataka maafisa mapato kusimama imara katika ukusanyaji wa mapato na yeye yupo nao bega kwa bega.
Ameyasema hayo, alipokuwa akizungumza kwenye kikao cha kujengeana uwezo baina ya maafisa mapato wa Halmashauri ya Jiji la Arusha na wale wa Jiji la Dar es Salaam.
Amewataka watumishi hao kutokata tamaa katika kukusanya mapato hata kama wanakutana na changamoto mbalimbali.
Amesisitiza kuwa kitendo cha kuongeza mapato kinasaidia Halmashauri kutekeleza majukumu yake kwa kiasi kikubwa hasa katika kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi.
Hamsini amesema mpango wa Halmashauri ni kukusanya leseni za biashara 30,000 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kutoka leseni 19,000 za sasa.
Ongezeko hilo litatokana na Halmashauri ya Jiji la Arusha kuanzisha ukusanyaji wa mapato kikanda kwa kuweka Vituo vya kukusanya mapato takribani 6 katika Jiji lote la Arusha.
Nae, Mwekahazina wa Jiji la Arusha Yoshua Myaluko amesema kikubwa ni kuweka juhudi katika ukusanyaji wa mapato na kufanya kazi kama timu.
Kutokana na mipango iliyopo ya Halmashauri ya Jiji la Arusha yakuongeza mapato na kuwarahisishia wananchi kupata huduma, Halmashauri itaanza kutoa huduma za biashara na kodi katika Vituo maalumu.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa