Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqaro amesema wanawake na vijana wanaokidhi vigezo wapewe Zabuni za Halmashauri ya Jiji ili kuweza kuwainua kiuchumi na kuboresha maisha yao kwa kazi mbalimbali zinazotolewa kila mwaka.
Daqaro ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya wanawake na vijana ambao ni wajasiriamali wanaonufaika na mikopo yenye riba nafuu kutoka Jiji ambayo hutolewa kwa mujibu wa sheria.
“Ni wakati wa wanawake na vijana kuchangamkia fursa mbalimbali katika Jiji la Arusha ikiwa ni pamoja na zabuni ambazo zitasaidia kuinua mitaji na kuongeza pato la familia zenu, hizi kazi ni zenu hakikisheni mnafuata taratibu zote ili mzichukue wasije watu toka mbali wakapewa wakati ninyi ambao ni wakazi wa Mji huu mkakosa kwa kukosa vigezo vidogo watumieni wataalamu wa Jiji wawaelimishe”amesema Daqaro.
Wakati akisema hayo Mkuu wa Wilaya Mhe. Daqaro amekabidhi hundi za mfano ya Tsh Mil 390 kwa vikundi vya wanawake 78 huku vikundi vya vijana 67 vimekabidhiwa hundi ya Tsh Mil 336.
Mhe. Daqaro amesema kuwa kutokana na changamoto iliyoko katika taasisi za fedha ambazo hutoa mikopo kwa riba kubwa na kuhitaji dhamana ya nyumba na ardhi jambo ambalo linawakwamisha wakopaji hivyo Serikali imeamua kutoa mikopo ya masharti nafuu ambayo ni asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Pia amewasihi wanufaika wa mikopo hii kuwa mikopo itumike katika malengo maalumu na katika miradi inatakayoleta tija kama vile uanzishwaji wa viwanda vidogo vidogo ambavyo vitasaidia kutengeneza ajira na kukuza uchumi.
Kwa upande wao kinamama na vijana waliopokea mikopo hiyo wamesema kuwa mikopo hiyo itawainua kiuchumi na kuwawezesha kufanya shughuli za uzalishaji mali na kuachana na kuwa tegemezi pamoja na matumizi ya dawa za kulevya na wizi.
Mpaka kufikia robo ya tatu Machi 2017 Halmashauri ya jiji la Arusha imetoa mikopo ya Tsh Bil 1.3 kwa ajili ya wanawake na vijana kwa mwaka wa Fedha 2016/2017.
Mwisho.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa