Mkurugenzi akabidhi msaada wa mipira kwa Timu ya AFC .
Na Mwandishi wetu
MKURUGENZI wa Jiji la Arusha Dk.John Pima amekabidhi mipira mitano kwa uongozi wa timu ya mpira ya Arusha Football Club ikiwa jitihada za kuunga mkono michezo katika Halmashauri ya Jiji la Arusha mpira wa miguu ukiwa miongoni mwa michezo hiyo.
Akikabidhi mipira hiyo kwa kiongozi wa timu ya AFC kocha Elly Kisanga alisema kuwa michezo ni burudani, ajira na kwamba Jiji la Arusha limepania kuhakikisha michezo inaendelezwa ikiwa ni pamoja na kuibua vipaji vya wachezaji.
Dk. Pima alisema viongozi wa Jiji la Arusha ambao ni Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mh.Kenan Kihongosi ,Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Matle Iranqhe ,Mbunge wa Jimbo la Arusha Mrisho Gambo wanajali na kuthamini michezo na kuwa nia ni kuona Halmashauri ya Jiji la Arusha inafanya vizuri kwenye michezo mbali mbali.
Kimsingi alisema Mh.Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.John Pombe Magufuli anapenda michezo na anatamani kuona Tanzania inafanya vizuri kwenye michezo kwamba watendaji wa Serikali jukumu lao ni kuhakikisha michezo husika inafanikiwa bila kikwazo.
Kwa upande wake Kocha wa Timu ya mpira Arusha (AFC) Elly Kisanga alimshukuru Mkurugenzi wa Jiji la Arusha na kuomba kuendelea kuwasaidia bila kuchoka na kuwaomba wadau wengine wa michezo kuunga jitihada alizoanza Dk.John Pima za kusaidia timu hiyo.
Kisanga alisema kuwa wako tayari kupokea msaada wowote kutoka kwa wadau ikiwa ni pamoja na chakula na kudai kuwa wakiwezeshwa watafanya vizuri na kuleta heshima ya mchezo wa mpira katika Jiji la Arusha.
Halmashauri ya Jiji la Arusha ni miongoni mwa Halmashauri ambazo zipo katika Mkoa wa Arusha ambao unahimiza michezo na tayari michezo mbali mbali imeanza lengo ikiwa ni kuibua vipaji vya wachezaji na hatimaye kuwapatia ajira kupitia michezo.
PICHANI MKURUGENZI WA HALMASHAURI YA JIJI LA ARUSHA DK. JOHN PIMA NA AFISA MICHEZO JIJI LA ARUSHA NDG. BENSON MANENO WAKIKABIDHI MSAADA WA MIPIRA KWA TIMU YA ARUSHA FOOTBALL CLUB (AFC)
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa