Halmashauri ya Jiji la Arusha leo tarehe 09/08/2019 imeketi kikao cha robo ya nne kwa mwaka wa Fedha 2018/2019 ambapo kwa mujibu wa kanuni kimepitisha taarifa za shughuli za maendeleo pamoja na kupokea taarifa kutoka katika Taasisi mbalimbali za serikali zinazotoa huduma kwa wananchi wa Jiji la Arusha.
Kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sekondari Arusha pia kiliambatana na zoezi la kumchagua Naibu Meya wa Jiji na uteuzi wa kamati za kudumu za Halmashauri, zoezi la uchaguzi wa Naibu Meya hufanyika katika kila robo ya nne ya kikao cha baraza la madiwani ambapo Mhe. Paul Mattysen, Diwani wa kata ya Moshono alifanikiwa kupita katika uchaguzi huo kwa mara ya pili.
Akifungua kikao hicho Mstahiki Meya wa jiji la Arusha ambaye ni Mwenyekiti wa baraza Mhe. Kalisti Lazaro Bukhay amepongeza juhudi zinazofanywa na Halmashauri katika kuwaletea wananchi maendeleo hususan harakati za Mkurugenzi wa jiji katika ukusanyaji na udhibiti wa mapato.
Sambamba na hayo Mhe. Kalisti aliendesha zoezi la uchaguzi wa wenyeviti wa kamati za kudumu za Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwemo Fedha na Utawala, Elimu, Maadili na Uchumi kwa mwaka huu mpya wa Fedha wa 2019/2020.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. Maulid Suleiman Madeni alipokuwa akitoa neno la shukrani alisema kuwa ushirikiano baina ya Viongozi, Madiwani na Watumishi ndio msingi wa kusogeza mbele gurudumu la maendeleo kwa wananchi wa Jiji la Arusha.
“Ningependa siku moja katika operesheni za ukusanyaji na udhibiti wa mapato ninazoziendesha niambatane na viongozi wa kisiasa pamoja na madiwani ili sote kwa pamoja tuweze kulinyanyua jiji hili kiuchumi ” alisema Dkt. Madeni
Miongoni mwa taasisi za kiserikali zinazotoa huduma kwa wananchi wa Jiji la Arusha zilizofanikiwa kuwasilisha taarifa ya utekelezaji ni pamoja na Wakala wa barabara za mijini na vijijini (TARURA), Mamlaka ya Mapato nchini Tanzania (TRA) pamoja na taasisi ya kifedha ya NMB.
Matukio mbalimbali ya mkutano wa baraza la madiwani
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa