Mkuu wa Mkoa awaonya Madiwani na viongozi ,wanaokwamisha mapato ya Halmashauri
Na Mwandishi wetu
MKUU wa Mkoa wa Arusha Idd Kimanta amesema hatakuwa tayari kuvumilia kuona kiongozi ama diwani anayekwamisha jitihada za maendeleo ikiwa ni pamoja na kukwamisha ukusanyaji wa mapato kutoka vyanzo vya mapato na kwamba viongozi kama hao watashughuliwa kwa mujibu wa sheria .
Mkuu wa Mkoa huyo ametoa onyo hilo wakati akifungua mafunzo ya madiwani ya siku tatu yakuwajengea uwezo na kujua majukumu yao kama wawakilishi wananchi katika Halmashauri ya Jiji la Arusha ,mafunzo yanayofanyika katika ukumbi wa mikutano ya Halmashauri ya Jiji la Arusha
Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha wanajukumu la kuhakikisha mapato yanakusanywa kutoka kwenye vyanzo vya mapato na kuonya kuwa ni marufuku kwa kiongozi kuhamasisha wananchi wasilipe mapato na kwamba Jiji la Arusha linahitajika kukusanya mapato hadi kufikia kiwango cha Tshs billion 22 zilipangwa kukusanywa za mapato ya ndani .
Aliwataka madiwani hao kufuata kanuni na sheria za Halmashauri pamoja na kuwa na mipaka katika utendaji na uwakilishi wa wananchi na kwamba mafunzo wanayowapatia yatawafungua na kuwafanya kujua mipaka yao .
Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha Kenan Kihongosi akimkaribisha Mkuu wa Mkoa kufungua mafunzo hayo aliwataka madiwani kuwa mfano bora na kuleta umoja katika Halmashauri ya Jiji la Arusha na kwamba wasiruhusu migogoro na migongano miongoni mwao .
Mh.Kihongosi alisema kuwa jukumu la madiwani ni kuhakikisha kuwa wanaletea wananchi maendeleo na kwamba maendeleo hayo yatapatikana kwa kuhimiza ukusanyaji mapato kama maagizo ya Serikali .
Alionya kauli na uchochezi wa baadhi ya viongozi wanaokwamishaji jitihada za kuhimiza wananchi kutekeleza wajibu wao wa kulipa kodi .
Kimsingi alisema kuwa agizo la Waziri wa TAMISEMI liko wazi kwamba ifikapo januari 30 mwaka 2021 kila Halmashauri iwe imekusanya mapato kufikia nusu ya mapato iliyojiwekea kukusanya mwaka wa fedha .
Naye Meya wa Jiji la Arusha Maxmillian Matle Iranqhe akizungumza kwa niaba ya madiwani hao alimhakikishia Mkuu wa Mkoa wa Arusha kuwa watashirikiana na Mkurugenzi wa Halmashauri pamoja na watumishi wa Halmashauri ya Jiji kukusanya mapato ya Halmashauri .
Alisema kuwa ni wazi kuwa umoja ni silaha na kuwa watashirikiana na watumishi wa halmashauri ya Jiji la Arusha kuwaletea wananchi maendeleo na kwamba Siasa zimekwisha .
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima akizungumzia mafunzo hayo alisema kuwa mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo Madiwani na wakuu wa Idara Halmashauri ya Jiji la Arusha kuendelea kujua majukumu yao .
Dk.Pima alisema kuwa baada ya mafunzo haya kila mshiriki atakuwa na uwezo wakujua wajibu na mipaka yake na hatimaye kufanya kazi za kuwatumikia wananchi kwa kufuata sheria na taratibu zilizopo .
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa