Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ndg. Humphrey Polepole amewataka Maafisa watendaji wa Kata kote nchini kushiriki katika vikao vya kamati za siasa za kata wakiambatana na watumishi wote katika kata zao pamoja na wataalamu kutoka katika taasisi zinazotoa huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwasilisha taarifa za maendeleo za kata husika.
Agizo hilo amelitoa leo Tarehe 07/2/2019 katika ziara yale ya kichama Jijini Arusha pamoja na kusherehekea miaka 42 ya kuzaliwa Kwa chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo alikagua ujenzi wa miradi ya huduma za wananchi ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Arusha Mjini iliyopo kata ya Engutoto, Ujenzi wa barabara ya Sombetini – FFU kipande cha kilometa 2.1, Ujenzi wa Madarasa manne Shule ya Msingi Murriet Darajani, ujenzi wa Maabara mbili katika Shule ya Sekondari Arusha Terrat pamoja na kuongea na Halmashauri Kuu za kata ya Engutoto, Lemara, Murriet, Terrat na Olasiti.
Polepole amesema kuwa ili kuimarisha ubora wa huduma za kijamii ni lazma watendaji wa kata nchini kote kushiriki vikao hivyo wakiambatana na watumishi wote katika kata sambamba na wataalam wa taasisi zinazotoa huduma za jamii ili kuweza kutoa taswira nzima ya maendeleo yanayofanyika katika kata husika huku wakiwa na majibu ya maswali na changamoto zote zitakazoibuliwa na wananchi.
“Watumishi wote nchini wanafanya kazi chini ya serikali ya CCM ambayo ndio ipo madarakani hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha ilani ya chama mnaisimamia kikamilifu katika kuwaletea wananchi wote maendeleo bila kujali itikadi zao za vyama, kisiasa na hata za kidini” alisema Polepole.
“Nikiwa kama mlezi wa Chama cha Mapinduzi katika Mkoa huu wa Arusha nichukue fursa hii kuupongeza uongozi wa Mkoa, ofisi ya Mkuu wa Wilaya, Halmashauri ya Jiji la Arusha pamoja na wataalam wake kwa matokeo mazuri ya mitihani ya Darasa la Saba, hakika mnanipa faraja na ninajivunia kuwa mlezi wenu” alongeza polepole.
Naye mmoja wa wakandarasi kutoka kampuni ya Sinohydro inayosimamia ujenzi wa barabara ya Sombetini – FFU kipande chenye urefu wa kilometa 2.1 chini ya Mradi wa Ukuzaji wa Miji na Majiji (TSCP) awamu ya tatu amesema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Machi mwaka huu kipande hicho cha barabara kitakuwa kimekamilika kwa kiwango cha lami na wananchi wataanza kunufaika na barabara hiyo.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa