Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi Kitengo cha usalama barabarani kuzidi kutoa elimu hasa kwa mitandao ya kijamii, kuwekeza katika utafiti na Maafisa wa polisi kujenga ukaribu na wananchi ili kupunguza ajali za barabarani.
Rais Samia ametoa maagizo hayo wakati wa ufunguzi wa Maadhimisho ya wiki ya Nenda kwa usalama barabarani yaliyo fanyika kitaifa Mkoani Arusha yatakayo dumu kwa wiki moja kuanzia Novemba 23 hadi Novemba 28, 2021 Ikiwa na lengo la kupunguza ajali za barabarani, huku Kauli mbiu yake Ikiwa ni '"Jali maisha yako na ya Mwingine Barabarani''.
"Mbali na kutumia runinga na vipindi vya redio, mnaweza kutumia mitandao ya kijamii kwasababu vijana wengi wapo huko hivyo mnaweza kuwafikia wengi zaidi...Lakini eneo la pili ni Utafiti ni vema mkafanya Utafiti ili mpate Suluhu ya kisayansi na kimfumo... askari muwe msaada kwa wananchi na si kuwa kero, muwe kimbilio la wananchi na sio mkimbiwe" -Rais Samia Suluhu Hassan.
Sanjari na hayo Rais Samia amejibu maombi kadhaa yaliyo wasilishwa mbele yake Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Wilbroad Mutafungwa, ombi la kupata Gawio la fedha za makusanyo ya Tozo Barabarani, mitambo ya kisasasa ya ukaguzi wa magari na camera katika barabara kuu.
Rais Samia amepinga ombi la Baraza la Usalama Barabarani kupata Gawio kutoka kwenye makusanyo ya Tozo akisema kuwa kwa kufanya hivyo Jeshi la polisi litatumia nguvu nyingi katika kutoza kitendo kitakacho bugudhi watumiaji wa Barabara.
Akiendelea kujibu ombi la mitambo ya kisasa ya ukaguzi wa magari, camera katika barabara kuu, Mh. Rais Samia ametoa mapendekezo kuwa Baraza la Usalama lifungue milango kwa sekta binafsi kuwekeza katika maeneo hayo kwani ni kwa muda mrefu sekta hizo zimekua zikihitaji nafasi hizo bila mafanikio.
Katika risala fupi iliyo wasilishwa na SACP Mutafungwa imeeleza kuwa Jeshi la Usalama barabarani limefanikiwa kupunguza ajali za barabarani akitoa takwimu kwa miaka minne tangu 2018 ambapo Mwaka 2018 jumla ya ajali zote ni 3732, Mwaka 2019 ni 2704, Mwaka 2020 ni 1714 na kwa mwaka 2021 ni 1388.
Maadhimisho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Majeshi, Wakuu wa Wilaya, Wabunge, Madiwani na Wengine huku Mwenyeji wao akiwa ni Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela. Mara ya mwisho Maadhimisho hayo yalifanyika Mwaka jana Mkoani Kilimanjaro.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa