Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh.John Mongela amewataka Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kushirikiana na watendaji wa Halmashauri kuhakikisha mapato yanakusanywa kutoka vyanzo vya mapato vilivyopo na pia kubuni vyanzo vipya.
Mkuu huyo ametoa kauli hiyo wakati wa Baraza Maalum la Madiwani lakujadili hoja za mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika Ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Mh.Mongella anasema kuwa Madiwani na wataalam wakishirikiana wataweza kuingia vyanzo vingi vya mapato na hivyo kupata fedha zakuendeleza miradi ya maendeleo hatimaye kuwaletea wananchi maendeleo.
Kimsingi alisema Jiji la Arusha linafanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato nakutaka Madiwani na wataalam kushikamana kwa kuhakikisha mapato yanaongezeka zaidi.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima akizungumzia maagizo hayo alisema kuwa tayari Wataalam na Madiwani wameanza zoezi la kufuatilia Mapato na kwamba kuna Matumaini ya mapato zaidi kuongezeka.
Dk.Pima alisema kuwa tayari vyanzo vipya vya mapato vimeanza kuanishwa ambapo amewataka wananchi kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.
Kwa upande wake Meya wa Jiji la Arusha Maximilian Iranqhe alisema kuwa Madiwani wa Jiji la Arusha wanamshikamano na kwamba suala la ukusanyaji Mapato litafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Mh.Meya alisema kuwa pamoja na kukusanya mapato pia wanaendelea na kampeni ya Usafi katika Jiji la Arusha ikiwa ni hatua yakufanya Jiji kuwa na hadhi ya Usafi hatimaye kuvutia wageni wa ndani na nje ya nchi.
Halmashauri ya Jiji la Arusha ni miongoni mwa majiji yanayofanya vizuri katika kukusanya mapato.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa