Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa Arusha John Mongela amesema hatawavumilia Waratibu wa Mpango wa kunusuru Kaya maskini (TASAF) ambao watabainika kuwa hawana uadilifu katika zoezi la kutambua wanufaika kutoka kaya masikini.
Mh .Mongela anasema kuwa baadhi ya Halmashauri nchini waratibu wanashindwa kutekeleza wajibu wao na kushindwa kutambua wanufaika halisi na kwamba katika Mkoa wa Arusha hatawavumilia waratibu kama hao.
Akizungumza katika kikao kazi cha kuwajengea uelewa Madiwani, Watendaji na Wawezeshaji wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kuhusu mpango wa TASAF kwa kipindi hiki cha pili katika awamu ya pili alisema kuwa waratibu wakiwa makini ni wazi kuwa miradi ya TASAF itatekelezwa kwa uadilifu.
Alisema kuwa hataruhusu kasoro zilizojitokeza kwenye awamu iliyopita zakuandikisha watu wasio na sifa nakuwataka waratibu kuwa makini katika kutambua kaya maskini.
"Niwasihi sana Wawezeshaji na waratibu kuongozwa na uzalendo na uadilifu katika kutekeleza majukumu yenu kwa ukaribu ili kuendeleza mazuri yote yaliofanyika awali kwa miaka 7 ya utekelezaji wa miradi ya TASAF.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha Dk.Sophia Mjema akimkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Arusha kufungua mafunzo hayo alisema kuwa ataungana na wataalam na waratibu wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika zoezi lakubaini wanufaika wenye Sifa.
Mh .Mjema alisema kuwa ni matamanio yake kuona kila mtu mwenye sifa anapata ruzuku ya mpango wa kunusuru kaya maskini na hatimaye kubadili hali yao ya maisha.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. John Pima alishukuru TASAF kwa kuipa upendeleo Halmashauri ya Jiji la Arusha na kutoa mafunzo pamoja kuzindua mpango huo kwa awamu ya Pili .
Dk.Pima alisema kuwa Halmashauri ya Jiji la Arusha itatekeleza kwa uadilifu zoezi lakutambua wanufaika wa mpango huo katika kata zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Mafunzo na semina hiyo imefanyika katika Ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa