RC Mongella akabidhi Mikopo ya Tshs million 640.9 kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu apongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Na Mwandishi wetu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongella amekabidhi Tshs milioni 640.9 ikiwa ni za mikopo kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu ikiwa ni sehemu ya mikopo ya asilimia 10 ya Fedha zinazotokana na Mapato ya ndani ya Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Mhe. Mongela akikabidhi mkopo huo katika ofisi za Kata ya Muriet, Tarafa ya Elerai alitaka wanufaika wa mikopo hiyo kutumia mikopo kwa kuanzisha shughuli zitakazobadili maisha yao na kuwa bora zaidi.
Mkuu huyo alitaka kurejesha mikopo hiyo kwa wakati hatimaye kuwezesha watu wengine kukopa na kujikwamua kutoka katika hali duni ya maisha.
Mikopo hiyo imetolewa na Halmashauri ya Jiji la Arusha ikiwa ya robo ya Tatu na ya Nne ikiwa imelenga vikundi 48 vya Tarafa ya Elerai ambavyo ni vikundi vya wanawake 34 vilivyopata mkopo wa Tshs Milioni 364.8, vikundi vya vijana 13 vimepatiwa Tshs Milioni 273.08 na kikundi kimoja cha watu wenye Ulemavu Tshs. Milioni 3.
Mhe. Mongella anasema fedha za mikopo hiyo zimetolewa na Serikali kwa lengo la kuwawezesha wananchi kuanzisha shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja ujasiriamali hatimaye waweze kuongeza kipato na kuondokana na umaskini.
Mkuu huyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwajali wananchi wake kuwa Mhe. Rais ametoa mikopo hiyo ikiwa ni kuwezesha wananchi anaowaongoza kuondokana na hali duni ya maisha baada ya kupata mikopo na kuanzisha shughuli za uzalishaji mali.
Amepongeza uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa kuendelea kutoa mikopo hiyo ambapo pia tayari Halmashauri hiyo imeweza kutoa mikopo kwa vikundi Tarafa ya Suye yenye thamani ya Tshs million 504.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk. Onesmo Mandike amesema kwamba Halmashauri itaendelea kutoa Mikopo hiyo kwa wakati na kutaka wananchi kujitokeza kuomba mikopo hiyo.
Kaimu Afisa Maendeleo ya Jiji la Arusha, Bi. Tajiel Mahega, akitoa ufafanuzi wa mikopo hiyo alisema Halmashauri ya Jiji itaendelea kutoa mikopo hiyo na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watu na wajasirimali wanaomba mkopo lengo ikiwa ni kuwawezesha kuanzisha Biashara zitakazobadili maisha yao kuwa bora na kuupa umaskini kisogo.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa