Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella ametoa siku tatu kwa wafanya biashara ndogo ndogo (machinga) kuhamia katika maeneo yaliyotengwa kwa kuanishwa kulingana na bidhaa wanazouza.
Aidha ametangaza eneo la Block E, lililopo kata ya Engutoto litumike kwa muda kwa malori kupakua na kupakia mizigo huku wakitafuta maeneo mengine kwaajili ya kupakia mizigo pamoja na virikuu watawekewa maeneo yao hapo baadae.
Mhe. Mongella alitoa agizo hilo leo eneo la Kilombero Jijini Arusha wakati alipokuwa akizungumza na wafanyabiashara wadogo (machinga) ambapo aliambatana na viongozi wa machinga pamoja na kamati ya ulinzi na usalama.
Alisema kuanzia siku ya Jumatatu, Jumanne na Jumatano Novemba 1-3 ,2021 wafanyabiashara hao wakahamie katika maeneo hayo yaliyotengwa ambayo ni Soko la Kilombero litakalokuwa linauza mboga mboga,matunda pamoja na bidhaa za chakula.
Ameongeza kwa kusema kuwa Soko la Mbauda litauza bidhaa zote za mitumba kila siku, soko la ulezi litauza nguo za dukani (spesho),Machame Luxury vifaa vya eletroniki pamoja vifaa vya nyumbani ikiwemo masufuria, Soko la Engutoto litakuwa ni kwaajili ya vifaa vya kuchomelea ikiwemo ,PVC,Vitanda,makochi na vitu vingine vinavyohusiana na bidhaa hizo huku Soko la Kwamromboo likitumika kwaajili ya minada ya nguo.
Alisema soko la Kilombero litatumika kuuza mboga mboga na kutoa rai kwa wafanya biashara hao kutumia masoko hayo kama watakavyopangwa kulingana na bidhaa wanazouza.
"Mtu asipotoshe kuhusu zoezi hili lenye tija kwa mslahi ya wananchi hawa na kama kunachangamoto ni lazima mawasiliano yawepo ili kuzitatua na usitokee upotoshaji" alisema Mhe. Mongella.
"Hatukatai changamoto tupeane taarifa ili tuzitatue,sisi sio malaika ni binadamu yawezekana katika zoezi hili tukaghafirika basi tushauriane na namshukuru Mwenyekiti wa Machinga Mkoa wa Arusha,Aminah Njoka na timu yake kwa ushauri wao tunashirikiana tuendelee kushirikiana" aliongeza Mhe. Mongella.
Mhe. Mongella alitoa rai kwa wafanyabiashara wenye uwezo wakafanye biashara katika maeneo yao waoiyopanga haya maeneo ni kwaajili ya machinga pekee ili wapate fursa ya kulipa sh,20000 kwa mwaka ili waweze kujikwamua kiuchumi kwa kuinuka na kuwa wafanyabiashara wakubwa hapo badae
Alisisitiza asitokee machinga akakimbilia eneo ambalo hajapangwa kila eneo lina mpangilio wake hivyo utaratibu utakuwepo chini ya usimamizi wa Jiji la Arusha kupitia kwa Mkurugenzi wa Jiji hilo, Dkt. John Pima na wataalam wake walioteuliwa kwa ajili ya kazi hiyo.
Kuhusu malori kupangwa alisema malori yote yatapakia na kushusha ndani ya wiki moja eneo la Engutoto kata ya Engutoto ambalo ni eneo la kuanzia na baadae watatafutiwa maeneo mengine ili waweze kupakia na kushusha kwani sasa hivi sasa malori hayana mpangilio kwaajili ya kupakia mizigo na kupakulia.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dkt. John Pima amemshukuru na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake ya kuhakikisha wanawapanga vema machinga hao na kwamba wao kama viongozi wapo tayari kuhakikisha zoezi hilo linaenda kufanyika kwa amani na utulivu kwa kufuata sheria na taratibu zote stahiki.
Naye Mwenyekiti wa wafanyabiashara ndogo Mkoa wa Arusha Bi. Aminah Njoka ameshukuru uamuzi wa Rais Samia Hassan Suluhu kwa kuwatoa wafanyabiashara hao juani na kuwaweka kivulini ili waweze kufanya biashara zao vizuri kulingana na sehemu zilizoanishwa huku akisisitiza machinga hao kuwa na imani na serikali kwani machinga hao kila mmoja atapata eneo la kufanya biashara zake
Bi. Njoka Alisema kila soko linabidhaa zake za kuuzwa hivyo wafanyabiashara hao watumie masoko hayo mapya kujikwamua kiuchumi kwani Jiji litakuwa miongoni safi na wananchi watajua wakitaka bidhaa fulani wanaipata wapi kulingana na uhitaji wao
Nao baadhi ya machinga waliishukuru uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa kwa hatua hiyo huku wakiiomba serikali kutenga maeneo mengine zaidi kwa wafanyabiashara watakaokosa maeneo kutokana na bidhaa wanazouza.
Mmoja kati ya wafanyabiashara hao, Jumanne Ismaili alishukuru uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa kwa uamuzi huo na kuomba wafanyabiashara hao kuuza bidhaa katika maeneo husika waliyopangwa.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa