Mkuu wa mkoa wa Arusha Mh. John Mongella amewataka wanaume kujitokeza kupima VVU ili kujua afya zao kwa mstakabali mzuri wa Familia zao na Taifa kwa ujumla.
Mh. Mongella ametoa wito huo alipokuwa akitoa nasaha zake kwa wana Arusha katika uwanja wa stendi ya daladala wa Kilombero Mkoani Arusha kufuatia maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani inayoadhimishwa Disemba Mosi kila mwaka.
RC Mongella amelitaja kundi la wanawake kuwa ndilo linaloongoza kwa upimaji wa VVU, huku wanaume wakibaki nyuma hivyo amewasihi wanaume kujitokeza kupima wajitambue ili ikiwa watakutwa na maambukizi waanze dozi za kufubaza virusi mapema ili waendelee kuhudumia wanaowategemea na Taifa.
"Nihamasishe wanaume tuunge mkono akina mama tukapime tujue afya zetu, baba na mama wakijua afya zao na kufuata masharti watasaidia sana jamii kwa kuendelea kutunza Familia na Taifa kupitia Uzalishaji mali" - RC Mongella.
Aidha amewataka vijana kujizuia kufanya ngono kabla ya wakati rasmi na wakishindwa kabisa watumie kinga ili kujinusuru na UKIMWI na magonjwa ya ngono.
Kufuatia kauli yake hiyo amewataka viongozi wa madhehebu kutokumuelewa vibaya katika hilo kwani wako waumini wasiotii na kuishia kupata VVU na kuziacha familia zikiteseja na kulipa Taifa hasara.
Awali akiwasilisha taarifa, Afisa Maendeleo ya Jamii Jiji la Arusha Bi. Tajiel Mahega ameeleza jitihada walizo tumia kupambana na maambukizi ya VVU mkoani Arusha ambazo ni pamoja na kuhamasisha kata 25 za Jiji la Arusha juu ya maambukizi ya VVU, kutoa elimu na ugawaji kondom 980,000 (KE) na (ME) katika vituo vya mabasi, Ofisi za kata na Idara zilizo katika Jiji la arusha.
Bi. Tajiel anaeleza kuwa licha ya jitihada zote zinazofanyika lakini maambukizi yameongezeka kutoka 2.3% kwa Mwaka 2019/2020 hadi 2.8% kwa Mwaka 2020/2021 na hii ni kutokana kuongezeka kwa idadi upimaji kwa makundi maalum mfano Vijana, Madadapoa na walio athirika na madawa ya kulevya na ufanisi katika upimaji.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa