Katibu Tawala Wilaya ya Arusha Ndg. David Mwakiposa kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha leo Tarehe 21 juni 2019 amekabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya Shilingi 397,500,000/= ambapo shilingi 190,000,000/= zimetolewa kwa vikundi 38 vya wanawake, shilingi 165,000,000/= kwa vikundi 29 vya vijana na shilingi 42,500,000/= kwa vikundi 9 vya watu wenye ulemavu kutoka katika kata 25 za Jiji la Arusha ikiwa ni mikopo ya robo ya nne kwa mwaka wa fedha 2018/2019.
Akifungua mafunzo ya ujasiriamali kwa vikundi hivyo Ndg. David Mwakiposa amesema kuwa ni serikali ya awamu ya tano pekee chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ndio imeweza kutenga asilimia 2 kwa watu wenye ulemavu kati ya asilimia 10 ya fedha za ndani za Halmashauri zinazotolewa kama mikopo ya kuwawezesha wananchi kiuchumi hivyo wananchi wanapaswa kuunga mkono jitihada za serikali na walengwa wa mikopo hiyo kuhakikisha wanarejesha fedha hizo kwa wakati ili ziweze kusaidia wengine.
Pichani: Walengwa wa mikopo wakipatiwa mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali mapema leo hii katika ukumbi wa Arusha School uliopo jijini Arusha. ********************* “Lengo la mikopo hii ni kuwawezesha wananchi kiuchumi, ni matamanio yangu siku moja wanufaika wapige hatua zaidi ili waweze kujitegemea na kuanzisha taasisi za kifedha kwa ajili ya kuinua watanzania wengine kiuchumi ili Taifa liweze kukua” Alisema Ndg. Mwakiposa.
Aliongeza kwa kutoa pongezi kwa Mkurugenzi wa jiji la Arusha Dkt. Suleiman Madeni pamoja na wataalamu wote wa Halmashauri kwa kuhakikisha fedha zinatengwa kwa ajili ya kuwainua wananchi kiuchumi na kuwapatia wanufaika wa mikopo hiyo mafunzo mbalimbali ya ujasiriamali.
Naye Kaimu Afisa Maendeleo ya jamii Jiji la Arusha Bi. Rahiya Nasoro amesema kuwa kwa sasa changamoto ya vikundi kutorejesha fedha kwa wakati imepungua kwa kiasi kikubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma hivyo wananchi wanapaswa kuendelea na moyo huo ili fedha hizo ziweze kusaidia wengine.
Mikopo hiyo inayotolewa kwa mujibu wa Sheria na miongozo imeelekeza asilimia kumi (10%) ya Mapato ya ndani ya Halmashauri kutolewe kama Mikopo isiyokuwa na riba kwa vikundi vya wanawake 4% , vijana 4% na watu wenye ulemavu 2%.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa