Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TASAF) jiji la Arusha umepongezwa kwa kutoa fursa kwa walengwa wanaonufaika na zoezi la uhawilishaji wa fedha kwa kaya masikini kuibua miradi ya ukarabati wa barabara katika mitaa saba ya jiji la Arusha.
Pongezi hizo zimetolewa kufuatia ziara ya kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha wakiambatana na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqarro pamoja na Katibu tawala wilaya ya Arusha Ndg. David Mwakiposa iliyofanyika jana tarehe 17/06/2019 lengo ikiwa ni usimamizi na utekelezaji wa ilani ya chama hicho katika ngazi ya Wilaya.
Akiongea wakati wa ziara hiyo Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya Ya Arusha Mhe. Joseph Massawe amesema miradi yote inayoendeshwa chini ya TASAF katika jiji la Arusha ni mfano wa kuigwa kwa halmashauri zote nchini kwani kwa licha ya kuwa inawasaidia wananchi masikini lakini pia imeweza kutoa fursa kwa walengwa wenyewe kuibua miradi ya ukarabati wa barabara katika mitaa 7 kati ya mita 70 inayonufaika na mpango wa uhawilishaji wa fedha katika jiji la Arusha.
Naye Mratibu wa TASAF jiji la Arusha Bi. Tajiel Mahega ameitaja mitaa inayohusika na miradi ya ukarabati wa barabara kuwa ni mtaa wa Kikwakaru B, mtaa wa Madukani, mtaa wa Oloresho, Mtaa wa Olmot Mateves, mtaa wa Mtoni, mtaa wa Block F na mtaa Viwandani.
“Miradi yote saba imefanyika katika ubora na ufanisi kwa kushirikiana na mafundi pamoja na walengwa wa mitaa husika ili kufanikisha ukarabati huo ambao unatarajiwa kukamilika tarehe 30/06/2019” alisema Bi. Tajiel
Sambamba na ziara hiyo pia kamati ya siasa ya Chama cha Mapinduzi (CCM) wilaya ya Arusha ilishuhudia zoezi la Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel Daqarro kukabidhi mradi wa ujenzi wa nyumba ya mwalimu wenye gharama ya shilingi milioni 62 pamoja na uzio wa shule ya msingi Suye uliogharimu shilingi milioni 85, ujenzi ulioanza mwaka 2018 mwezi wa 9 chini ya mradi wa TASAF awamu ya tatu.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa