“Tukigawanyika tunatengeneza mianya yakupoteza rasilimali zetu na hivyo kutufanya Watanzania tuwe maskini”.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Felician Mtahengerwa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paulo Makonda katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanzania, yaliyofanyika Jijini Arusha.
Mtahengerwa amesema, Muungano huo umesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto mbalimbali kwa pande zote na hivyo kurahisha kupatikana kwa maendeleo kirahisi.
Amesema, tusikubali kuuvunja muungano huu kwani nchi nyingi ambazo zimevunja muungano wao nchi hizo zimejikuta zimeingia katika migogoro na zinatamani kurudisha muungano wao ili waishi kwa amani.
Aidha, amewataka wananchi wa Mkoa wa Arusha kuendelea kuulinda muungano huo kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
Kupitia Muungano wetu tumeweza kufanya maendeleo mengi ikiwemo ujenzi wa shule nyingi za Sekondari na Msingi, mradi wa TASAF wa kutokomeza umaskini, ujenzi wa vituo vingi vya afya, miundombinu ya Barabara inaendelea kuimarika kila siku.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa Bwana Missaile Musa amesema kutokana na kauli mbiu ya mwaka huu inayosema “Tumeshikamana na tumeimarika kwa maendeleo ya Taifa letu”, hivyo tuendelee kushikamana na kuimarika kwa maendeleo ya Taifa letu.
Maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano kimkoa yamefanyika sambamba na shughuli za kijamii kama vile kufanya usafi, kupanda Miti na utoaji wa Damu salama , vyote hivi vimefavyika katika Hospitali ya Wilaya ya Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa