Katika utekelezaji wa mkakati wa kutangaza utalii wa ndani Kanda ya Kaskazini leo tarehe 04/09/2019 Halmashauri ya Jiji la Arusha imeendeleza kampeni ya Talii Kaskazini kwa kushirikisha wanafunzi wa shule ya msingi Arusha School ambapo walitembelea Makumbusho ya elimu ya viumbe, Themi Living Garden, Mnara wa Saa (clock tower) na makao makuu ya Jiji la Arusha ambapo walijifunza historia ya Jiji na vivutio vya utalii vilivyopo Jiji la Arusha.
Kampeni ya Talii Kaskazini ina lengo la kuhamasisha utalii wa ndani na inajumuisha mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Tanga na Manyara.
Kwa mujibu wa Afisa Utalii Jiji la Arusha Michael Ndaisaba ameeleza kuwa kampeni hiyo imeanzia katika Jiji la Arusha kwa kuhamasisha wanafunzi kwani licha ya kuwa ni sehemu ya mafunzo bali pia ni wadau wakubwa wa kuhamasisha utalii wa ndani katika jamii.
Ndaisaba amesema kuwa kampeni ya Talii Kaskazini inalenga kukuza mahusiano ya taasisi zinazohusika na utalii na zitakazoshiriki kutekeleza mkakati huo wa kutangaza utalii wa ndani kanda ya Kaskazini, kukuza uelewa wa vivutio vya utalii kwa wakazi wa kanda ya Kaskazini kwa kuwekeza kwenye utalii wenye gharama nafuu na kwenye maeneo ambayo ni rahisi kufikika, kukuza utamaduni wa kupenda utalii kwa vijana hasa wanafunzi na kuongeza idadi ya watalii wa ndani kufikia 2,000,000 ifikapo mwaka 2021.
Kampeni ya Talii Kaskazini inashirikisha wadau mbali mbali wa masuala ya utalii nchini wakiwemo Tanzania Tourist Board (TTB), Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Mamlaka ya wasimamizi wanyamapori (TAWA) na wengineo.
Walengwa wa mkakati huu ni wakazi wa Kaskazini mwa Tanzania wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo, waajiriwa kwenye taasisi mbalimbali za kiserikali na zisizo za kiserikali, taasisi za kifedha, wafanyabiashara, vikundi mbalimbali vya jamii na wananchi wa kawaida.
“HII NI TANZANIA ISIYOSAHAULIKA; UTALII WA NDANI UNAANZA NA WEWE, TWENDE TUKATALII”
Wanafunzi wa shule ya msingi Arusha School wakipatiwa historia ya Jiji na kujifunza vivutio vya utalii vilivyopo Jiji la Arusha
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa