VIJANA wametakiwa kuwa chachu ya kufikisha elimu ya UVIKO-19 kwa makundi sahihi ili makundi hayo yaweze kupata Chanjo hiyo na kutakiwa kupuuzia Habari za upotoshaji za mitandaoni na kwamba chanjo hiyo ni salama.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Dk. Sophia Mjema katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani iliyofanyika katika viwanja vya michezo vya Ngarenaro vilivyopo Jijini Arusha.
Mhe. Mjema amesema kwamba takribani asilimia 77 ya watanzania ni vijana na kwamba ndio kundi linalotegemewa katika maendeleo ya nchi ya Tanzania hivyo wanapaswa kuwa mabalozi wazuri kwa Jamii kwa kuwahimiza kushiriki kikamilifu zoezi la uchomaji Chanjo ya UVIKO-19 ili Jamii iwe salama na ugonjwa huo.
'' Kama mnavyofahamu vijana sasa ni asilimia 77, iliyobakia ni ya Wazee kwa hiyo vijana sasa ndio mnaotegemewa kuleta maendeleo ya nchi yetu'' amesema Mh. Mjema.
Kimsingi Mh. Mjema amewataka Vijana kupuuzia Habari za upotoshaji mitandaoni kwa madai kwamba chanjo hiyo sio salama na kusisitiza kuwa Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suhulu Hassan imekuwa inawajali wananchi wake.
"Upotoshaji ulikuwepo ninyi vijana naomba mkaufute kwa sababu ukipata chanjo ya UVIKO-19 utajikinga na kuwakinga na wengine" aliongeza Mh. Mjema.
Naye Diwani wa kata ya Lemara Mhe. Naboth Silasie akimwakilisha Mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Maxmillian Iranqhe amesisitiza umuhimu wa afya bora kwa vijana na kutoa wito kwa wazazi wa Vijana hasa watoto wa kike kupata vipimo vya afya ikiwemo kufanyiwa uchunguzi wa Saratani ya shingo ya kizazi.
Maadhimisho hayo ya siku ya vijana duniani yalipambwa na mada mbali mbali za kuwajengea uwezo, michezo na bidhaa wanazozizalisha vijana hao.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa