Na Mwandishi wetu.
WADAU wa Elimu Halmashauri ya Jiji la Arusha wametakiwa kuwa makini kudhibiti wizi wa mitihani kwamba hakuna mwanya wa kurudia mitihani kwa shule zitakazobainika kuiba mitihani.
Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Dk.John Pima anawataka kudhibiti udanganyifu katika mitihani ya mwisho katika shule zao ikiwa ni pamoja na kuzingatia maelekezo ya Serikali yanayotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa.
Wadau na Wataalam hao ni Wamiliki wa Shule, Wakuu wa Shule, Maafisa elimu kata, Wenyeviti na wajumbe wa bodi za shule ambao walishiriki katika Mkutano maalum Uliofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Sekondari Edmund Rice Sinon uliopo Jijini Arusha.
Dkt. John Pima amesema kwamba udanganyifu katika mitihani una madhara na unasababisha mtoto kupoteza ndoto ya kuendelea na masomo yake kwa wakati.
"Msimamo wa Serikali kama kuna shule imejulikana kuwa imefanya udanganyifu katika mitihani, matokeo yakifutwa kwa darasa hilo, hawana nafasi nyingine ya kufanya mitihani. Kwa hiyo tumekuwa tumesababisha hasara kwa watoto Wenyewe na Serikali kwa Ujumla" alisema Dkt. Pima.
Aidha, Dkt Pima kwa kushirikiana na Kamati ya Mitihani ya Wilaya wamekuja na mkakati uitwao "No Zero Program" wenye lengo la kutokomeza sifuri katika shule zote za Serikali na binafsi zilizopo Halmashauri ya Jiji la Arusha huku akiwataka wadau hao kushirikiana na walimu mashuleni kwao kwa kuhakikisha matokeo ya kidato cha pili, cha nne na sita hakuna mwanafunzi atakayepata alama sifuri.
Pamoja na mambo mengine, Dkt. Pima amewataka wadau hao kufuata maelekezo ya Serikali kwa kuchukua tahadhari zote mapema na kugundua mapema viashiria kwa kutoa taarifa juu ya majanga ya moto na majanga mengine mbalimbali katika shule zao na sio kusubiri mpaka majanga hayo kutokea huku akiwataka pia wadau hao kuendelea kuchukua tahadhari juu ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO19) kwa kufuata miongozo inayotolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
Naye Afisa Elimu Msingi Jiji la Arusha, Ndg. Omary Kwesiga akizungumza katika Mkutano huo alimshukuru Dkt. Pima kwa maelekezo yake na kwamba ni jukumu lao sasa kuyafanyia kazi ili kuhakikisha Jiji la Arusha linaenda kufanya vizuri zaidi katika Shule za Msingi na Sekondari kwani nia wanayo uwezo wanao.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa