Wataalamu wa afya katika Jiji la Arusha wametakiwa kuendelea kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele kwa kuhamasisha na kuelimisha jamii juu ya umuhimu huo pamoja na kutekeleza zoezi la kitaifa la umezaji wa dawa kinga tiba ya minyoo kwa watoto wenye umri wa miaka 5 – 14 kila mwaka.
Agizo hili limetolewa na mkuu wa Wilaya ya Arusha mapema leo Tarehe 12 Machi 2020 katika ufunguzi wa zoezi hilo linalotarajiwa kufanyika katika shule 48 za msingi zilizo za Serikali na 106 zisizo za Serikali katika Halmashauri ya Jiji la Arusha .
Ufunguzi wa zoaezi umefanyika leo Tarehe 12 Machi katika shule ya msingi Daraja mbili na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Gabrieli Daqarro akiambatana na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ambaye pia ni Afisa elemu msingi Mhe. Omar Kwesiga na Diwani wa Kata ya daraja mbili Mhe. Msofe , Mganga Mkuu wa Jiji Dkt. Herry Kagya pamoja na timu ya uwezeshaji huduma za afya kutoka Halmashauri ya Jiji la Arusha (CHMT).
Akifungua zoezi hilo Mkuu wa Wilaya ya Arusha alisema kwa mwaka 2019 zoezi hilo lilifikia asilimia 92 ya utekelezaji wake na lengo kuu la mwaka huu 2020 ni kufikia asilimia 100 ambapo wanafunzi 104,986 Jijini wakiwa wavulana 52,771 na wasichana 52,215 wanatarajiwa kumeza dawa za minyoo.
Zoezi hilo litasimamiwa na walimu 3,083 na wataalamu wa afya 170 pia alisisitiza zoezi hilo likafanyike kwa ufanisi na aliwasihi waalimu waendelee kuwaelimisha watoto kuzingatia usafi wa mazingira na vyoo kwani baadaye wao ndio watakua mabalozi wazuri katika jamii.
Pia alimpongeza afisa elimu na walimu wote wa Shule ya msingi Daraja mbili kwa kuongoza kufaulisha kwa miaka miwili mfululizo kitaifa katika matokeo ya mitihani ya taifa darasa la nne na kuwaomba wataalamu wa afya wahahakikishe kuwa wanatokomeza magonjwa ambayo yalikua hayapewi kipaumbele katika Jamii .
Naye Afisa elimu msingi Mhe. Ommar Kwesiga Alishukuru Serikali kwa utoaji huduma mbalimbali za kijamii na alipongeza juhudi za Mhe.Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutoa elimu bure na kuboresha miundombinu ya shule kwani imeleta mafanikio makubwa katika sekta ya elimu.
Kadhalika diwani wa kata ya Daraja mbili Mhe.Msofe alimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Arusha kwa kufungua zoezi hilo la umezaji dawa kinga tiba ya minyoo kwa niaba ya Jiji zima la Arusha katika Kata yake .
Sambamba na hilo naye Mganga Mkuu wa wa Jiji la Arusha Dkt. Kheri alisema mwaka 2015 katika jiji la Arusha ugonjwa wa minyoo ulikua kati ya yale magonjwa 10 yanayoongoza lakini hadi hivi sasa wamesha punguza kwa kiasi kikubwa na zoezi hilo limeanza kuzoeleka katika jamii na Halmashauri ilikwisha kusaini (M.O.U) tangu tarehe 31/01/2020 yenye jumla ya bajeti ya Tshs 40,965,102.21/= ambazo ni ruzuku kutoka Wizara ya Afya kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserekali kama vile (USAID) kwaajili ya ufanikishaji wa zoezi hilo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo katika ngazi mbalimbali, kuratibu shughuli za uhamasishaji, matangazo na usimamizi wa vifaa. Pia alitoa rai kwa watanzania hususani wazazi, waruhusu watoto wao wapate dawa hizo ambazo ni salama kwa watoto wao.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa