Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Eng. Joseph Nyamhanga amehudhuria zoezi la kuapishwa kwa watumishi saba walioteuliwa kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 leo Tarehe 12 Septemba 2019 Jijini Arusha.
Watumishi hao walioteuliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Suleiman Jaffo (MB) kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa mkoa wa Arusha ni Msena Nyamwiling’i Bina, Mkuu wa idara ya utumishi na utawala halmashauri ya Jiji la Arusha, Hussein Ramadhan Mgewa, Mkuu wa idara ya elimu msingi halmashauri ya wilaya ya Arusha, Pius John Haule, Mkuu wa kitengo cha uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Karatu, Natang’adauki Zakayo Mollel, Mkuu wa idara ya elimu msingi halmashauri ya wilaya ya Longido, Jonathan Peter Kima, Mkuu wa kitengo cha sheria halmashauri ya wilaya ya Meru, Theresia Evarist Kyara, mkuu wa idara ya mipango, takwimu na ufuatiliaji halmashauri ya wilaya ya Monduli na Emmanuel Joseph Mhando, mkuu wa idara ya utawala na utumishi halmashauri ya wilaya ya Ngorongoro.
Zoezi la kuapisha watumishi hao limeongozwa na Hakimu Mkazi wilaya ya Arusha Mhe. Pendo Mushi.
Sambamba na zoezi la kuapishwa, watumishi hao walikabidhiwa vifaa vya uchaguzi ambavyo ni Tangazo la uchaguzi wa serikali za mitaa, kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa, Muongozo wa uchaguzi wa serikali za mitaa na ramani ya mipaka.
Akizungumza baada ya kuapishwa kwa wasimamizi hao Eng. Nyamhanga ameiagiza sekretarieti ya mkoa wa Arusha, wakurugenzi wa halmashauri na makatibu tawala wa wilaya kusimamia zoezi la uchaguzi wa serikali za mitaa kikamilifu na kuwapa ushirikiano mzuri wasimamiza wa uchaguzi wa serikali za mitaa. Pia ameagiza migogoro baina ya wananchi na viongozi itatuliwe na amani idumishwe katika jamii ili kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika na kumalizika vyema.
Pichani: Msena Nyamwiling’i Bina, Mkuu wa idara ya Utumishi na Utawala Halmashauri ya Jiji la Arusha akiapishwa
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa