Na Mwandishi Wetu
ARUSHA.
Imeelezwa kuwa iwapo Watendaji wa Mabaraza ya Kata watatimiza majukumu yao ipasavyo kwa kuzingatia Sheria, taratibu, na kanuni zinazowaongoza ni wazi kuwa wananchi wataiamini serikali yao na kwamba serikali haitasita kuwachukilia hatua wale wote watakaoenda kinyumbe na kukandamiza haki za wananchi.
Akizungumza na wajumbe wa mabaraza hayo pamoja na watendaji wa Kata zote za Jijini Arusha katika wiki ya sheria, Mkurugenzi wa Jiji hilo Dkt. John Pima amesema kwa kuwa wananchi wengi wapo ngazi za chini kwa maana ngazi ya Kata hivyo ni wazi kuwa utendaji kazi wao ndiyo utakaoirahisishia serikali katika kutumikia wananchi.
Amesema serikali haitarajii kuona watendaji hao kuwa chanzo cha migogoro na kwa kutambua umuhimu wao halmashauri ya Jiji hili imetenga fedha kwa ajili ya kuwapatia mafunzo ya siku mbili yatakayowasaidia kufanya kazi kitaalamu zaidi ikiwa ni pamoja na kuwapunguzia wananchi gharama ya muda na fedha katika kushughulikia mashauri yao.
“Ninyi ni kiungo muhimu sana kati ya serikali na wananchi, kupitia ninyi wananchi wataiamini serikali yao iwapo mtawajibu ipasavyo, hivyo ili kuboresha utendaji kazi wenu tumewaandalia mafunzo ya siku mbili ambapo pamoja na mambo mengine yatawasaidia kujua mipaka yenu ya kazi” Alisema Dkt Pima.
Hata hivyo alisema kuwa pia watatoa elimu kwa wananchi juu ya uendeshaji wa mashauri ikiwemo namna ya upelekaji wa utetezi kwani uzoefu unaonyesha kuwa wengi wao hawana elimu hiyo hali inayopelekea malalamiko mengi kwa madai kuwa hawakutendewa haki.
Kwa upande wake Naibu Msajili Mahakama Kuu Arusha Mhe. Judith Kamala amewaambia wajumbe hao kuwa mabaraza ya Kata yapo kisheria na kwamba kwa mujibu wa sheria mpya ijulikanayo kama Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Namba 3 ya mwaka 2021 imeyataka Mabaraza ya Ardhi ya Kata kutoa usuluhishi na siyo hukumu kama ilivyokuwa hapo awali.
Ameongeza kusema kuwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia pia Sheria hiyo imeelekeza kuwepo kwa mjumbe mwakilishi mwanamke miongoni kwa wajumbe watatu wanaounda baraza la usuluhishi na kwamba shauri lolote linatakiwa kumalizika ndani ya siku 30 tu.
Akizungumzia muundo, sifa pamoja na majukumu ya mabaraza hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Ardhi na Nyumba Wilaya ya Arusha Gladness Kagaruki aliwasisitiza wajumbe hao kutofautisha kati ya migogoro ya ardhi na ya mirathi.
“Licha ya sheria kusema ni lazima kuwepo kwa mjumbe mwanamke kwenye baraza la usuluhishi lakini hata wajumbe wote wakiwa ni wanawake sheria haikatazi, bali tunawasistiza msichanganye mirathi na migogoro ya ardhi, na pia ninyi hamna haki kisheria ya kugawa mali, watu wakija kwa ajili ya mirathi waelekezeni mahakamani” Alisema Kagaruki.
Baadhi ya wajumbe hao Mohammed Abdallah kutoka Kata ya Unga Ltd, Richard Mollel kutoka Kata ya Elerai, Raphael Tinde kutoka Kata ya Sombetini pamoja na Fredy Laizer kutoka Kata ya Muriet wamesema mafunzo hayo ni ya kwanza tangu wamekuwa katika nafasi hizo kwa muda wa zaidi ya miaka mitano sasa na kwamba hata hiyo sheria mpya walikuwa hawaifahamu na ndiyo maana wamekuwa wakiendelea kutoa hukumu badala ya usuluhishi licha ya kwamba sheria hiyo ilianza kutumika toka tarehe 11/10/2021.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa