Mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe. Gabriel F. Dagarro amefungua kikao cha maandalizi ya mipango ya bajeti cha afua za lishe ambacho kimehudhuriwa na wakuu wa idara mbalimbali wa Halmashauri ya Jiji pamoja na wawakilishi kutoka wizara ya afya katika kikao kilichofanyika kwenye ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha mapema leo Tarehe 12 Desemba 2019.
Akifungua kikao hicho Mhe.Dagarro amewasihi watoa huduma za afya kutoa elimu ya kutosha juu ya afya ya lishe kwa mama wajawazito pamoja na elimu juu ya malezi ya mtoto baada kuzaliwa na kuhakikisha mtoto ananyonyeshwa ndani ya miezi sita ya mwanzo.
Sambamba na hayo Mhe. Daqarro ameelekeza katika kliniki kuwepo na maafisa lishe watakao toa elimu kuelekeza kuwa katika suala la upimaji wa afya watoto wapimwe vizuri ili kuvumbua matatizo mengine yanayowakumba kutokana na ukosefu wa lishe bora kwani lishe bora hujenga vyema afya ya ubongo na mwili wa mtoto.
Akiwasilisha takwimu kwa mgeni wa heshima afisa lishe wa Jiji Bi.Rose Mauya amesema kiwango cha udumavu ni asilimia 31.8 kitaifa kwa mwaka 2018 na kwa mkoa wa Arusha udumavu umepungua kutoka asilimia 36 hadi kufikia asilimia 25.2 kwa mwaka 2018.
Pia Bi.Rose ameainisha changamoto zinazokabili kitengo cha lishe kuwa ni baadhi ya wazazi kutozingatia umuhimu wa unyonyeshaji wa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo na wahudumu wa afya ya msingi kutokua na elimu ya kutosha ya upimaji wa maswala ya lishe.
Licha ya kuwepo kwa changamoto Bi. Rose amesema kitengo cha lishe kimefanikiwa kuongeza kiwango cha utoaji wa matone ya vitamin A na dawa za minyoo kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kufikia asilimia 97.5, kufanya usimamizi shirikishi katika vituo vya afya 6 na dispensary 4, kufanya upimaji wa lishe kwenye shughuli za maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji na mwenge na kutembelea shule 8 za msingi na kutoa elimu kuhusu lishe pamoja na kufanya upimaji wa hali ya lishe.
Aidha afisa mwandamizi kutoka wizara ya afya Ndg.Peter Kaswahili ameiasa jamii kuzingatia unyonyeshaji wa mtoto ndani ya miezi 6 ya mwanzo ili kumkinga na maradhi mbalimbali pamoja na kumjenga afya na akili .
Hata hivyo Bi. Joyce Ngegba ambaye ni afisa lishe kutoka UNICEF ameainisha sababu za utapiamlo katika jamii kuwa ni ulaji duni, maradhi, ukosefu wa chakula katika kaya, huduma duni za jamii, utunzaji duni wa makundi maalumu, ukosefu wa huduma za afya kwa jamii, uchafuzi wa mazingira, mifumo mibaya ya siasa ,vitapamoja na mila na desturi potofu.
Mwisho.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa