Waziri Kairuki: Halmashauri fuateni miongozo ya utekelezaji wa miradi.
Na Mwandishi Wetu
Arusha.
Waziri wa Nchi OR-TAMISEMI Mhe. Angellah Kairuki amezitaka Halmashauri zote nchini kufuata maelekezo kwa mujibu wa namna zilivyowafikia na kufuata taratibu za manunuzi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuepuka hoja za ukaguzi kwani kwa kufanya hivyo itakuwa na kurudisha nyuma kazi kubwa inayofanywa na Serikali.
Waziri Kairuki ameyasema hayo leo Disemba 13,2022 alipokuwa akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa timu za utekelezaji wa mradi wa BOOST unaolenga kuboresha mazingira ya ufundishaji na Ujifunzaji ndani ya Nje ya Shule kwa Elimu ya awali na Msingi ngazi ya Mikoa na Halmashauri hafla iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa shule ya sekondari Ilboru ya Mkoani Arusha.
Mhe. Kairuki amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali za Halmashauri ambao pia ni wasimamizi wa miradi kutokwenda kinyume na maelekezo ili kuepuka kupoteza muda na kuleta migogoro na mifarakano isiyo ya lazima.
"Nitoe rai kama unaona kuna namna nzuri ya kutekeleza kabla ya kubadilisha basi Wasiliana na TAMISEMI kwa maelekezo sahihi, kwa maana dhana ya ushirikishwaji ni jambo la muhimu ili kuepuka sintofahamu zisizo za lazima" amesema Waziri Kairuki.
Katika hatua nyingine amezielekeza Halmashauri kufuata taratibu stahiki za manunuzi ili kuepuka hoja za ukaguzi, akiwasisitiza kutekeleza usimamizi bora wa fedha na mapato.
Naye Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI Ndg Ramadhan Kailima amesema kuwa Mradi wa BOOST ni wa miaka 5 (Mitano) 2021/2022 hadi 2025/2026 wenye lengo la kuboresha mazingira ya ufundishaji na Ujifunzaji ndani ya Nje ya Shule kwa Elimu ya awali na Msingi utagharimu kiasi cha Shilingi Trilioni 1.15 kwa ujenzi wa Madarasa 12,000 nchi nzima.
Aidha, Ndg. Kailima amependekeza kila Halmashauri izingatie maelekezo ya mradi huo wa BOOST na kuwa ikiwezekana uwe ajenda ya kudumu kwenye Timu za Uongozi (CMT) pamoja na Baraza la Madiwani.
Awali, Mkurungenzi wa Elimu (TAMISEMI) Ndg. Vincent Kayombo akitoa taarifa fupi ya mradi huo amesema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi mbalimbali ili kuwezesha kufikia malengo yanayotakiwa.
Mafunzo hayo ya Mradi huo wa BOOST yanafanyika Mikoa yote 26 na Halmashauri zote 184 shule za serikali na jumla ya Washiriki 274 watapatiwa mafunzo hayo ya siku mbili nchi nzima.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa