Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye amesema kuwa Jiji la Arusha ni miongoni mwa majiji yatakayonufaika na zoezi la anuani za makazi baada ya kuingizwa katika mfumo maalum wa lugha za mataifa mbalimbali utakaowezesha watalii kujua majina ya mitaa na kupata huduma muhimu.
Aidha amewaomba viongozi wa dini kuisaidia serikali katika utoaji wa elimu ya anuani za makazi ili kufungua fursa za kimaendeleo za ndani na nje ya nchi ya Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa Habari Mkoani humo, Mhe. Nnauye alisema mkoa huo ni miongoni mwa mikoa inayofanya vema katika zoezi la anuani za makazi.
Hivyo alitoa rai kwa Wakala wa Barabara Mijini na Vijiji (TARURA)na Wakala wa Barabara (TANROADS)kushirikiana kwa pamoja na Wizara ili kuhakikisha zoezi hilo linakamilika.
Alisema Mkoa wa Arusha mara baada ya zoezi hilo kukamilika utakuwa ni miongoni mwa mikoa yenye manufaa zaidi baada ya majina ya mitaa kuingizwa katika mifumo ya anuani za makazi kwaajili ya kuwezesha sekta ya utalii kukua kwani watalii watakuwa wanaangalia majina ya mitaa na kujua aina za huduma watakazozipata kupitia lugha mbalimbali za mataifa yao.
Alisema pia ni vema katika zoezi la uwekaji majina katika mitaa mbalimbali waangalie historia za viongozi na watu mbalimbali mashuhuri wakiwemo watafiti ili wakumbukwe kwa majina yao kuandikwa katika mitaa mbalimbali kwaajili ya kutambua michango yao waliyoitoa kwa jamii mbalimbali au nchi.
"Wekeni majina ya watu walitumikia mambo mbalimbali katika historia ya nchi yetu ili watoto wetu wajue historia zao , kunawatu nchi hii wamefanya mema na historia zao zikumbukwe pia Arusha mtanufaika na anuani za makazi sababu ya fursa za utalii zilizopo maeneo haya"
Aliwaomba viongozi wa dini mbalimbali kutoa elimu katika nyumba za ibada ili waumini wajue umuhimu wa anunani za makazi na fursa zilizopo katika kujipatia maendeleo
"Nawapongeza Mkoa wa Arusha kwaubunifu wa karakana hii itakayosaidia uwepo wa nguzo na naomba mikoa mingine kuiga mfano huu wa kutengeneza nguzo za chuma kwaajili ya anuani za makazi"
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Dkt. Jim Yonazi alipongeza ubunifu uliofanywa na Mkoa wa Arusha kwa kuanzisha karakana ya kutengeza nguzo na kusisitiza kuwa awali kulikuwa na changamoto za mfumo lakini hivi sasa mfumo upo vizuri kwa ajili ya kuhakikisha zoezi hilo linakwenda kama lilivyopangwa.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongella alisema kuwa kwa Mkoa wa Arusha wametumia changamoto za ukosefu wa fedha kama fursa za kutatua changamoto zilizopo katika kuhakikisha Mkoa wa Arusha na Jiji la Arusha kwa ujumla linahakikisha zoezi la anuani za makazi linakwenda vema kwani timu zimegawana kila wilaya na halmashauri za mkoa huo kwaajili ya kuhakikisha zoezi hilo linakwenda kama walivyojipangia kumaliza
"Mkoa huu unatumia fursa za anuani za makazi ili kujikwamua kiuchumi na wananchi wanatoa ushirikiano sasa tunaomba msiwe na wasiwasi Arusha hii ni ya mfano kwa anuani za makazi"
Awali Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda akitoa tathimini ya zoezi hilo alisema hadi sasa zoezi la uwekaji anuani za makazi linaendelea vema hadi sasa wameshakamilisha zoezi hilo katika kata 21 kati ya 25 zilizopo Jiji la Arusha.
Alisema pia majengo yameshakamilika na wamepanga kufanya tathimini ya maeneo ambayo hawajayafikia pia hadi sasa wameweka nguzo 2,130 kati ya nguzo 9,554 zinazohitajika na kuongeza kuwa hadi sasa wameanzisha karakana ya kutengeneza nguzo hizo ili kukidhi mahitaji ya nguzo yanayohitajika.
Alisema walikaa chini na kutathimini changamoto kama fursa ikiwemo kufanya mazungumzo na wadau mbalimbali wa viwandani ili waweze kupata ndoo zaidi ya 200 za rangi.
"Arusha hatuhitaji kusema tunaupungufu wa fedha bali tunatumia upungufu huo kama fursa za kujikwamua ili kuhakikisha zoezi hili linamalizika kwa wakati"
Naye Said Mabie ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi ,Mipango na Uratibu Mkoa wa Arusha ,alisema zoezi hilo kwa Mkoa wa Arusha lilianza April 12,2022 na viongozi mbalimbali walishirikishwa na walianza kuweka alama maeneo mbalimbali na kusema kuwa mkoa huo ulipokea sh,milioni 905 .63 kwaajili ya kutekeleza zoezi hilo na walianza kutoa elimu kwa umma kuhusu zoezi la anuani za makazi ikiwemo wataalam kupewa elimu.
Alisema kwa Jiji la Arusha zoezi hilo limekamilika kwa asilimia 78.7 na Halmashauri ya Monduli ni asilimia 45.82 , Ngorongoro asilimia 12.51, Arusha DC asilimia 11.21,Meru Dc asilimia 4.2 , Karatu asilimia 2.59 na Longido ikiwa ni asilimia 39.04
Alimalizia kwa kuishukuru Serikali kwa kuongeza sh. milioni 10 kwaajili ya kutatua changamoto hizo ikiwemo changamoto ya mfumo wa utoaji wa anuani za makazi na kusisitiza zoezi hilo linatarajia kukamilika Mei 31 mwaka huu lakini Mkoa wa Arusha unakamilisha zoezi hilo Aprili 30 mwaka huu.
Matukio katika picha ni Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Nnauye akiongozana na Viongozi wa Mkoa wa Arusha wakati akikagua utekelezaji wa zoezi la anwani za makazi Jijini Arusha, leo Aprili 12, 2022.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa