Halmashauri ya Jiji la Arusha yapokea tuzo kwa Kushika nafasi ya pili kitaifa katika mashindano ya usafi wa Mazingira ya mwaka 2019.
Wizara ya Afya, maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto ikishirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI imekuwa ikiratibu mashindano ya usafi wa Mazingira na kwa mwaka huu mashindano hayo yamefanyika na washindi wamepatikana kwa ngazi mbalimbali ambapo Jiji la Arusha limeshindanishwa katika kundi la Halmashauri za Majiji na Manispaa 25 ambapo Jiji la Arusha limeshika nafasi ya Pili nakupata asilimia 90.8 ikiongozwa na Halmashauri ya manispaa ya Moshi iliyoshika nafasi ya kwanza kwa kupata asilimia 91.5 na Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kushika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 78.
Tuzo hii imetunukiwa na waziri wa Afya,maendeleo ya Jamii jinsia wazee na watoto Mhe. Ummy Mwalimu katika maadhimisho ya wiki la usafi wa mazingira na mkutano wa maafisa Afya wa mikoa, Halmashauri na wadau uliofanyika Tarehe 16-18 Desemba 2019 katika ukumbi wa Landsmark Jijini Dodoma na kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni “Huduma bora za Afya mazingira na usafi ni kichocheo muhimu cha uchumi endelevu”
Afisa Afya na Mazingira Jiji la Arusha Bw. James Lobikoki amebainisha kuwa Jiji limeendelea kushika nafasi hii ya pili kwa kipindi kingine mfululizo kwani kwa mwaka 2018 Jiji la Arusha lilishika nafasi ya pili katika mashindano ya majiji hivyo kwa mwaka huu mashindano hayo yamechukua sura mpya na kuboreshwa zaidi hivyo mchuano kuwa mkali kwani sio tu kushindanishwa na majiji bali kwa Halmashauri za majiji na manispaa 25.
Ndg . James ameeleza kuwa mashindano haya yanafanyika kwa kuzingatia vitu vingi ikiwa ni pamoja na kuzingatia usafi wa mazingira kwa ujumla, uzoaji na usafirishaji wa taka, ushirikishwaji wa Jamii na vikundi mbalimbali na taasisi katika suala la usafi wa mazingira, bajeti inayotengwa kwaajili ya suala zima la usafi wa mazingira, uhifadhi salama wa taka, upatikanaji wa maji safi na salama, ujenzi wa vyoo na matumizi ya vyoo pamoja na usafi wa vyoo hivyo.
Sambamba na hilo Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru iliyopo Jijini Arusha imeshika nafasi ya kwanza katika kundi la Hospitali za Mikoa nchini pia katika kundi la hospitali za binafsi Hospitali ya “Arusha Lutheran Medical Center” imeshika nafasi ya kwanza na katika kundi la Hoteli "Kibo Palace Hotel" nayo imeshika nafasi ya kwanza katika hoteli zote nchini pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Arusha nayo vilevile imeshika nafasi ya pili katika kundi la ofisi za wakuu wa mikoa.
Mwisho.
Pichani: Naibu Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Poul Matthysen akipokea tuzo ya Afya, Usafi na Mazingira kwa niaba Halmashauri ya Jiji la Arusha.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa