Mkuu wa wilaya ya Arusha Mhe. Said Mtanda amewataka wananchi hasa makundi ya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kutumia fursa ya uchukuaji wa mikopo ya asilimia 10 kwa lengo la kujiinua kiuchumi wao binafsi na nchi kwa ujumla.
DC Mtanda (Katikati) akiwa ameshika Hundi ya Tsh. Milioni 404.5 ambayo alikabidhi kwa vikundi wanufaika.
Mhe. Mtanda ameyasema hayo Jijini Arusha,wakati akizungumza na Vikundi Wanufaika wa Mikopo hiyo ambapo amesema kuwa zaidi ya Sh.milioni 143 zitatolewa kwa vikundi vya vijana 14 lakini wengi wao hulalamika mikopo hiyo haiwafikio kitokana na kutokupata taarifa.
"Lakini wanapopewa mikopo wahusika pengine hawaioni hivyo ni vyema tukaendelea kuwaonyesha kwamba sisi Jiji la Arusha kwamba tunatekeleza sera na maelezo ya serikali ya kutoa asilimia 10 ikiwa vijana asilimia 4,wanawake asilimia 4 na 2 kwa watu wenye ulemavu,"alisema Mtanda.
"Jumla ya vikundi 52 ambapo vikundi vingi ni vya kinamama vitapatavyo 28 baada ya kupata majibu ya vikundi vingi kuwa ni vya kinamama nilibaini kuwa ni wanawake ni wahaminifu pindi wanapopewa mikopo" aliongeza Mtanda.
Alisema wanawake hao wanatengeneza mazingira ya kujikomboa kiuchumi ikiwemo vikundi vya watu wenye ulemavu ambapo serikali imewarahisishia sio lazima kuwepo katika vikundi bali wanatoa hata kwa mtu mmoja mmoja.
"Mtu yeyote mwenye ulemavu aliyetayari katika kujikwamua kiuchumi anapewa mikopo hata akiwa peke yake kwa hiyo sisi tunaamini kila mtu anaweza akiwezeshwa na hawa tunataka wawe mfano kwa walemavu wengine kwani wanao uwezo mkubwa na nguvu,"alisema Mkuu huyo.
Mtanda alitoa wito kwa vikundi vyote vinavyopokea mikopo kuwa waadilifu kwenye mikopo hiyo ili waweze kuaminika na ni lazima wawe na utamaduni wa kulipa marejesho ya mikopo hiyo ya Halmashauri na wasijiwekee matumizi mabaya.
Mkuu huyo alisema kama ni kikundi ni vyema kikawa na maendeleo ya pamoja kwani ikumbukwe kuwa umoja ni nguvu utengano ni dhaifu.
Naye Kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya Jiji la Arusha,Hergeney Chitukuro alisema katika kipindi cha robo ya mwaka wametoa mikopo yenye jumla ya sh.milioni 873.6 kwa jumla ya vikundi 108.
"Lakini katika kipindi hiki tumetoa mikopo ya awamu ya pili katika vikindi 52 ambapo vimepata jumla ya sh.milioni 404.5 ikiwa mchanganuo wake ni vikundi 28 ni wanawake ambao wamepata sh.miliono 198.6,vijana vikundi 14 vimepatiwa jumla ya sh.milioni143 na watu wenye ulemavu ni vikundi 10 ambapo wamepatiwa jumla ya sh.milioni 62.9,"alisema Chitukuro.
Naye Mbunge wa Arusha mjini Mrisho Gambo ameushukuru uonhozi wa halmashauri ya jiji la Arusha kwa kuwapatia mikopo wanufaika hao kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kuhakikisha wanapata mikopo kama serikali ya awamu ya sita inavyoelekeza.
Wanufaika wa Mikopo wakishiriki katika semina ya mafunzo ya kujengewa uelewa juu ya mikopo ya asilimia 10 iliyofanyika kwenye Ukumbi wa Arusha School.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa