Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mwita Waitara (Mb) leo Tarehe 27/04/2019 amefanya ziara katika jiji la Arusha kwa lengo la kutembelea miradi ya elimu na kuongea na watumishi wa kada ya elimu pamoja na makao makuu ya jiji la Arusha.
Katika ziara yake Mhe. Waitara ametembelea ujenzi wa jengo la utawala na matundu 6 ya vyoo katika shule ya sekondari Suye na kuangalia maendeleo ya ujenzi unaotokana na fedha za mpango wa elimu kwa matokeo (EP4R) wenye thamani ya shilingi milioni 56 ambapo alipongeza namna ujenzi unavyokwenda vizuri.
Sambamba na ziara yake pia Mhe. Waitara alipata fursa ya kuongea na watumishi wa kada ya elimu pamoja na makao makuu ya jiji la Arusha ambapo alisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika miradi ya maendeleo.
“Serikali inatoa fedha nyingi kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezeka hususan ya elimu hivyo rai yangu kwa viongozi wa halmashauri ni kuwashirikisha wananchi ili wawe sehemu ya maendeleo ya miradi hiyo” alisema Naibu Waziri huyo
“Licha ya wananchi kujiona ni sehemu ya miradi lakini pia nirahisi wao kujua ni nini serikali inafanya katika maeneo yao na itawapelekea wao kuitunza na kuithamini miradi hiyo” aliongeza mhe. Waitara.
Sambamba na hayo pia Mhe. Waitara amesisitiza fedha zinazopelekwa katika halmashauri zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa na endapo kutatokea vipaumbele vingine vinavyopelekea kubadili matumizi ya fedha hizo au fedha zisipokidhi mahitaji ya miradi husika basi taarifa ipelekwe mapema katika wizara husika ili kukwepa hoja za ukaguzi endapo miradi itashindwa kutekelezeka au kukamilika.
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa