Mkuu wa wilaya ya Arusha Mjini Mhe. Gabriel Daqaro amewataka wazazi na walezi kuwaleta wototo wote ambao hawajakamilisha chanjo za utotoni na wale walio hasi chanjo katika vituo vya afya vinavyotoa chanjo ili kupatiwa huduma muhimu ya chanjo inayotolewa bure nchi nzima.
Ameyasema hayo leo tarehe 06/05/2019 wakati akizindua zoezi la wiki ya chanjo katika kituo cha afya Ngarenaro kilichopo kata ya Levolosi jijini Arusha, ambapo zoezi hilo linatarajiwa kumalizika tarehe 12/05/2019.
“Lengo la zoezi hili ni kuwafikia watoto wote ambao hawakukamilisha au hawajakamilisha chanjo za utotoni hivyo niwaombe wazazi na walezi kujitokeza kwa wingi katika vituo vyetu vya afya mkiwa na watoto wenu ili waweze kukamilisha chanjo zote zinazohitajika kwa mujibu wa sheria na Sera ya afya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania”. Alisema Mhe. Daqarro
Naye Mratibu wa Chanjo Jiji la Arusha Bw. Didas Misana amesema kuwa zoezi la wiki ya chanjo kwa watoto hufanyika kila wiki ya mwisho wa mwezi Aprili kila mwaka, lengo ni kuwakinga watoto dhidi ya magonjwa kama surua, kifadulo, dondakoo, pepopunda, nimonia, polio (ugonjwa wa kupooza), magonjwa ya kuharisha kwa watoto na ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 14.
“Zoezi la chanjo linahusisha watoto wenye umri kuanzia miezi sifuri hadi miaka mitano isipokuwa chanjo ya ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi inahusisha wasichana waliokamilisha umri wa miaka 14 ” alisema Bw.Didas
Vituo vyote vinavyotoa huduma ya chanjo vitakuwa vikifunguliwa kuanzia saa moja na nusu asubuhi na kufungwa saa kumi na nusu jioni. Na kauli mbiu ya mwaka huu inasema
“ CHANJO NI KINGA KWA PAMOJA TUWAKINGE ”
20 Boma Street 23101
Sanduku la Posta: 3013
Simu: 0272548072
Simu ya Mkononi: 0272545768
Barua Pepe: cd@arushacc.go.tz
Haki Miliki ©2018 Halmashauri ya Jiji la Arusha .Haki zote Zimehifadhiwa